DAR ES SALAAM:
Serikali ya Tanzania imesema iko tayari kushirikiana na wawekezaji kutoka Qatar kuendeleza fursa za uwekezaji katika sekta za mifugo na uvuvi, hususan uzalishaji na usindikaji wa nyama, sekta ya kuku pamoja na miundombinu ya uvuvi.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, Agosti 31, 2026, wakati wa mazungumzo na Naibu Waziri Mkuu wa zamani wa Qatar, Dkt. Khalid bin Mohammad Al Attiyah, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Thirty-Five Investment Holding.
Dkt. Kakurwa amesema Tanzania ina uwezo mkubwa wa kuzalisha nyama na tayari imeongeza mauzo ya nje kutoka takribani tani 1,000 mwaka 2021 hadi karibu tani 15,000 kwa sasa, huku ikilenga kufikia tani 50,000 kwa mwaka.
Amesema Serikali inahitaji ushirikiano na wawekezaji katika kuimarisha uzalishaji, usindikaji, uongezaji thamani na viwango vya bidhaa ili Tanzania iweze kuongeza zaidi mauzo ya nyama katika masoko ya Qatar na Mashariki ya Kati.
Katika sekta ya uvuvi, Waziri huyo amesema Serikali inapendekeza ushirikiano kati ya Kampuni ya Uvuvi Tanzania (TAFICO) na Thirty-Five Investment Holding, akitaja fursa zilizopo katika uvuvi wa bahari kuu, usindikaji na uongezaji thamani wa mazao ya uvuvi.
Kwa upande wake, Dkt. Al Attiyah amesema yuko tayari kuendelea na majadiliano kuhusu fursa hizo, ikiwemo uwekezaji katika miundombinu na mnyororo mzima wa thamani wa sekta ya uvuvi.
