MULEBA, KAGERA.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Mwang’onda, amempongeza Meneja wa TARURA Wilaya ya Muleba, Mhandisi Dativa Telesphory, kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa wilayani humo.
Mwang’onda ametoa pongezi hizo wakati wa ziara ya Mwenge wa Uhuru wilayani Muleba, akisema usimamizi madhubuti wa miradi ni muhimu katika kuhakikisha fedha za Serikali zinatumika ipasavyo na kuleta matokeo kwa wananchi.
Amesema Mhandisi Dativa, ambaye pia ni Mratibu wa Mwenge wa Uhuru wilayani humo, ameonesha mfano mzuri wa namna wataalamu wanavyoweza kutumia taaluma zao kuchochea maendeleo.
“Napenda kumshukuru na kumpongeza Meneja wa TARURA wilayani Muleba kwa kazi nzuri anayoifanya. Wahandisi wengine wajitolee kama alivyo Mhandisi Dativa ili kusaidia kuharakisha maendeleo,” amesema Mwang’onda.
Aidha, amewataka viongozi na watendaji wilayani Muleba kuendelea kusimamia kwa umakini miradi inayotekelezwa katika maeneo yao, akisisitiza kuhakikisha kila fedha inayotolewa na Serikali inazaa matokeo yenye manufaa kwa wananchi.

