Arusha.
Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhe. Mwinyi Ahmed Mwinyi ameiomba Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge Uratibu na Wenye Ulemavu ikamilishe Sera ya Taifa ya Ufuatiliaji na Tathmini kwa ubora unaostahili, kwa ushirikishwaji wa Serikali pamoja na wadau ili kuweka msingi wa pamoja wa kitaasisi, kitaalamu na kiutendaji wa mfumo wa ufuatiliaji na tathmini nchini.
Mhe. Mwinyi ameyasema hayo kwa Niaba ya Waziri wa Nchi, Prof. Mpalamagamba Kabudi, Waziri Wa Nchi – Ofisi Ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) wakati wa halfa ya kufunga Kongamano la Tano la Kitaifa la Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza leo tarehe 25 Septemba, 2026 Jijini Arusha.
“Ninasisitiza maelekezo aliyotolewa na Mhe. Waziri Mkuu katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba na Mhe. Daniel Barran Sillo, Ofisi ya Waziri Mkuu iendelee kuharakisha na kukamilisha Sera ya Taifa ya Ufuatiliaji na Tathmini kwa ubora unaostahili na kwa ushirikishwaji wa serikali nzima pamoja na wadau, ili kuweka msingi wa pamoja wa kitaasisi, kitaalamu na kiutendaji wa mfumo wa M&E nchini na hili niongeze msisitizo kuwa kongamano lijalo lifanyike huku likiambatana na uzinduzi wa Sera hiyo amesisitiza Mhe. Mwinyi.
Aidha, Mhe. Mwinyi ameitaka Ofisi ya Waziri Mkuu (SBUU) kuendelee kushirikiana na Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kukamilisha Muundo wa Utumishi wa Kada ya Ufuatiliaji na Tathmini, ili kada hiyo iwe na majukumu yaliyowazi, viwango vya kitaaluma na mwelekeo wa maendeleo ya kiutumishi.
“Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa na taasisi za utoaji huduma ziendelee kuimarisha kliniki za uwajibikaji na majadiliano ya kiutendaji, ili changamoto za wananchi zibainishwe na kutatuliwa katika ngazi zinazowahudumia” ameongeza Mhe. Mwinyi.
Vilevile, Mhe. Mwinyi amesisitiza maazimio yaliyofikiwa katika Kongamano hilo yasiishie kuwa kumbukumbu ya mkutano bali Sekretarieti ya Kongamano, chini ya uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, iyatafsiri katika mpango wa utekelezaji unaoonesha hatua, taasisi inayowajibika, muda wa utekelezaji na viashiria vya kupima maendeleo.
Aidha, ameongeza kuwa “masuala yaliyojitokeza katika Kongamano hili yameendelea kuonesha umuhimu wa kukamilisha Sera ya Taifa ya Ufuatiliaji na Tathmini; kuimarisha Muundo wa Utumishi wa Kada ya Ufuatiliaji na Tathmini; kuendeleza Mfumo Jumuishi wa Kielektroniki wa Ufuatiliaji na Tathmini; kuimarisha rasilimali na uwezo wa vitengo vinavyosimamia Ufuatiliaji na Tathmini; na kuhakikisha kuwa taarifa na ushahidi unaozalishwa kupitia Ufuatiliaji na Tathmini unatumika kikamilifu katika vikao vya menejimenti, upangaji, bajeti na maamuzi ya kiutendaji”.
Mbali na hayo Dkt. Yonazi amewashukuru viongozi mbalimbali wa Serikali, viongozi wa Mkoa wa Arusha na Wilaya ya Arumeru, TanEA, taasisi za elimu na utafiti, wadau wa maendeleo, vyama na mitandao ya kitaaluma, sekta binafsi, asasi za kiraia, waoneshaji, wawezeshaji, wanahabari pamoja na washiriki wote kutoka ndani na nje ya nchi kwa mchango walioutoa katika kufanikisha Kongamano hilo.


