Dar es Salaam
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeanza rasmi maandalizi ya kuanzisha huduma ya upandikizaji wa moyo nchini, hatua inayotarajiwa kuimarisha huduma za kibingwa na kutoa matumaini mapya kwa wagonjwa wenye matatizo makubwa ya moyo.
Maandalizi hayo yanafanyika kwa ushirikiano na wataalamu kutoka Misri na Kuwait, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa JKCI wa kujenga uwezo wa ndani kupitia mafunzo ya wataalamu wa afya, uandaaji wa miongozo ya matibabu na kuweka mazingira wezeshi yatakayowezesha huduma hiyo kuanza kutolewa kwa ufanisi.
Akizungumza katika kikao cha pamoja cha utekelezaji wa mpango huo, Mkurugenzi wa Huduma za Tiba kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Hamad Nyembea, alisema Serikali imeanza kutekeleza mpango huo kama sehemu ya juhudi za kupanua huduma za kibingwa na ubingwa bobezi nchini, sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Dkt. Nyembea alisema hatua hiyo inaonesha dhamira ya Serikali ya kuendelea kuimarisha sekta ya afya kwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma za matibabu ya kiwango cha juu ndani ya nchi bila kulazimika kusafiri nje ya Tanzania.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Naizihijwa Majani, alisema kuanzishwa kwa huduma ya upandikizaji wa moyo ni hatua muhimu katika safari ya taasisi hiyo ya kupanua wigo wa huduma za matibabu ya moyo.
Alieleza kuwa JKCI imebaini kuwepo kwa kundi la wagonjwa ambao mioyo yao imeshindwa kabisa kufanya kazi na ambao kwa sasa hawapati huduma hiyo nchini, hali inayowalazimu kutafuta matibabu nje ya nchi au kukosa huduma stahiki.
“Kuanzishwa kwa huduma hii kutaleta matumaini mapya kwa wagonjwa hao na kuongeza uwezo wa nchi katika kutoa matibabu ya moyo ya kiwango cha juu,” alisema Dkt. Majani.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi za Kiarabu, Mhe. Balozi Mohand Salah Ladjouzi, alisema ushirikiano huo kati ya Tanzania na nchi za Kiarabu unalenga kuwajengea uwezo wataalamu wa Kitanzania kupitia mafunzo ya vitendo na kubadilishana uzoefu, hatua itakayosaidia kuimarisha ujuzi wa kitabibu na ubora wa huduma za afya nchini.
Mpango huo unatarajiwa kuiwezesha Tanzania kujiunga na nchi chache barani Afrika zinazotoa huduma ya upandikizaji wa moyo, huku ukiimarisha zaidi nafasi ya JKCI kama kituo kinachoongoza katika huduma za matibabu ya moyo katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

