Marubani wa ndege nyuki maliasili wapigwa msasa

Na Sixmund Begashe, 

Manyoni.

WIZARA ya Maliasili na Utalii kupitia Mfuko wa Kuhifadhi Wanyamapori Tanzania (TWPF), inaendesha Mafunzo maalumu ya matumizi ya ndege nyuki (Drone) kwa Marubani zaidi ya 50 ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa kudhibiti changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu katika maeneo ya wananchi. 

Akizungumzia jitihada zinazofanywa na Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Mhe. Vincent Mashinji, ameipongeza Wizara hiyo kwa kazi nzuri inayofanyika katika kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu hususani katika Wilaya ya Manyoni. 

Ameongeza kuwa ofisi yake itaendelea kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii katika uhifadhi wa maliasili zilizopo Manyoni kwa maslahi mapana ya wananchi na taifa kwa ujumla. 

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni Bi. Anastazia Tutuba amesema kufanyika kwa mafunzo hayo Manyoni kutasaidia wataalam kupata uelewa mpana wa matumizi ya teknolojia ya kisasa ya ndege nyuki ili kuimarisha udhibiti wa wanyamapori wakali na waharibifu na kuepusha madhara kwa wananchi na mali zao. 

Mafunzo hayo yanayohudhuriwa na marubani wa ndege nyuki kutoka, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongo ( NCAA) na Idara ya Wanyapori (WD), yanaendeshwa na kampuni ya Uhusiano International ICT Ltd kwa kushirikiana na wataalamu wa Wizara ya Maliasili na Utalii.