Kigali, Rwanda
Serikali ya Tanzania imeendelea kuimarisha mifumo ya kudhibiti utakasishaji fedha haramu, ufadhili wa ugaidi na ufadhili wa silaha za maangamizi, hatua inayolenga kuongeza ulinzi wa sekta ya fedha na kuimarisha mazingira ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, amesema hayo jijini Kigali, Rwanda, wakati wa Mkutano wa 26 wa Baraza la Mawaziri la Umoja wa Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika wa Kupambana na Utakasishaji Fedha Haramu, Ufadhili wa Ugaidi na Silaha za Maangamizi (ESAAMLG).
Amesema Tanzania imefanikiwa katika tathmini ya pamoja (Mutual Evaluation) iliyofanywa na ESAAMLG kupitia Kamati ya Wataalamu, huku Serikali ikiendelea kushughulikia maeneo yaliyobainishwa ili kuboresha zaidi mifumo ya nchi katika mapambano dhidi ya vitendo hivyo.
“Tuna sheria na kamati ya kitaifa ya kupambana na masuala haya. Mafanikio ni makubwa, lakini bado kuna maeneo 15 tunayafanyia kazi, ikiwemo marekebisho ya sheria 12 zilizobainishwa kuwa zinahitaji maboresho kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar,” amesema Balozi Omar.
Amesema kwa upande wa Tanzania Bara, sheria nne tayari zimepitishwa na Bunge katika kikao kinachoendelea, huku Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikitarajiwa kuwasilisha miswada ya kurekebisha sheria nyingine tatu, hatua itakayosaidia kukamilisha maboresho yanayohitajika.
Balozi Omar amesema hatua hizo zimewezekana kutokana na ushirikiano wa taasisi mbalimbali nchini, zikiwemo Wizara ya Fedha, taasisi zinazosimamia sekta ya benki, Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Mambo ya Ndani pamoja na taasisi nyingine zinazoshiriki katika Kamati ya Kitaifa ya kupambana na utakasishaji fedha haramu na vitendo vinavyohusiana na ufadhili wa ugaidi.
Mkutano huo umewakutanisha Mawaziri, Makatibu Wakuu na maafisa waandamizi kutoka nchi wanachama wa ESAAMLG kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika kudhibiti utakasishaji fedha haramu, ufadhili wa ugaidi na ufadhili wa silaha za maangamizi.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo umejumuisha Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Homera; Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Dkt. Seif Abdallah Shekalaghe; Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango-Zanzibar, Bw. Aboud Hassan Mwinyi; na Kamishna wa Kitengo cha Ujasusi wa Fedha (FIU), Bw. Majaba Magana.
Wengine ni Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania na Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Wataalamu ya Kuzuia Utakatishaji Fedha Haramu, Bi. Sauda Msemo, pamoja na wakuu wa taasisi, wataalamu wa sekta ya fedha, wasimamizi wa taasisi za kifedha na wadau wa maendeleo kutoka Tanzania na nchi nyingine.


