Dar es Salaam
MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeongeza kasi ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati katika Bandari ya Dar es Salaam, ikilenga kuongeza uwezo wa kuhudumia meli na mizigo, kupunguza msongamano pamoja na gharama zinazotokana na ucheleweshaji wa meli. Miongoni mwa miradi hiyo ni ujenzi wa Tank Farm yenye matanki 15 ya kisasa, unaolenga kupunguza muda wa meli kukaa bandarini kutoka siku 21 hadi takribani siku saba.
Akizungumza wakati wa ziara ya viongozi wa serikali za wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali, Mkurugenzi wa Huduma za Uhandisi TPA, Mhandisi Eric Madinda, alisema meli itahudumiwa kwenye gati kwa saa 24 na muda uliobaki ikiwa nangani, hatua inayotarajiwa kupunguza gharama za demurrage zilizokuwa zikifikia takribani Dola 25,000 kwa siku. Alisema kupungua kwa gharama hizo kutasaidia kupunguza gharama zinazomfikia mlaji kupitia bei za bidhaa.
Madinda alisema TPA inaandaa awamu ya pili ya Tank Farm itakayoongeza matanki zaidi, huku ikipanga kujenga gati jipya eneo la Kendo lenye uwezo wa kuhudumia hadi meli nne kwa wakati mmoja zenye uzito wa tani 150,000 hadi 200,000. Pia kuna mipango ya kuhamisha Kurasini Oil Jetty (KOJ) na kujenga magati namba 12 hadi 15 ili kuongeza uwezo wa bandari.
Aidha, alisema TPA inaendelea kushirikiana na wadau kuboresha usafirishaji wa mizigo kutoka bandarini kupitia SGR na MGR, pamoja na mipango ya kujenga barabara za kulipia kutoka bandarini kuelekea Kibaha na Morogoro. Hatua hizo zinalenga kupunguza msongamano wa malori na kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo.
Kwa upande wake, Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Ardhi (ARISU), Osward Beatus Maganya, aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Wizara ya Uchukuzi kwa uwekezaji katika Bandari ya Dar es Salaam. Alisema kuongeza urefu wa magati kutoka mita 120 hadi zaidi ya mita 500 na kina cha bandari kufikia mita 15 kumeongeza uwezo wa kupokea meli kubwa, huku kuunganishwa kwa SGR na MGR na bandari kukisaidia kupunguza utegemezi wa malori.
Naye Makamu wa Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DARUSO), Kasti Karen Mary, aliishukuru Wizara ya Uchukuzi kwa kuwawezesha wanafunzi kujifunza kwa vitendo kuhusu maendeleo ya sekta ya bandari. Alisema sekta hiyo ina mchango mkubwa katika uchumi wa Tanzania na kuwataka vijana kuchangamkia fursa za ajira, biashara, ubunifu na uwekezaji zinazotokana na miradi hiyo, huku akimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia utekelezaji wa miradi ya kimkakati.
