DAR ES SALAAM
WAHITIMU wa Chuo cha Bandari wametakiwa kutumia ujuzi na weledi walioupata chuoni hapo kuongeza ufanisi katika sekta ya bandari na uchukuzi wa majini, ili kuchangia kufikiwa kwa malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.
Wito huo umetolewa Jijini Dar es Salaam wakati wa kongamano la pili la wahitimu wa Chuo cha Bandari lililowakutanisha wahitimu na wanafunzi wanaoendelea na masomo chuoni hapo, kwa lengo la kujadili mchango wa wataalamu katika kukuza sekta ya bandari na uchukuzi wa majini.
Akizungumza katika kongamano hilo, Katibu Mtendaji wa Chama cha Mawakala wa Meli Tanzania (TASAA), Abel Estomihi Uronu, amesema maendeleo ya sekta ya bandari yanahitaji nguvu kazi yenye ujuzi wa kutosha, sambamba na uwekezaji katika teknolojia na miundombinu ya kisasa.
Uronu amesema sekta binafsi inatarajiwa kuchangia takriban asilimia 70 ya pato la taifa (GDP), hivyo wataalamu wanapaswa kuwa na uwezo wa kuendesha mitambo na kusimamia shughuli za bandari kwa ufanisi.
Amevitaka vyuo vinavyotoa mafunzo ya sekta hiyo, ikiwemo Chuo cha Bandari, DMI na NIT, kuimarisha mafunzo ya vitendo pamoja na uzingatiaji wa sheria, kanuni na taratibu za kazi ili kuzalisha wataalamu wanaokidhi mahitaji ya soko.
Amesema uhaba wa wataalamu wenye weledi unaweza kusababisha ucheleweshaji wa mizigo, hasara na uharibifu wa mali, hali inayoweza kuathiri viwanda vya ndani na nchi jirani zinazotumia bandari za Tanzania.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Wahitimu wa Chuo cha Bandari, Robert Jonathan Melami, amesema uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika miundombinu ya bandari unapaswa kwenda sambamba na uwepo wa wataalamu wenye uwezo wa kusimamia na kuendesha shughuli zake.
Melami amesema kukua kwa bandari nchini na kuongezeka kwa shehena za mizigo kumeongeza mahitaji ya wataalamu na washauri katika sekta ya usafirishaji wa majini.
Amebainisha kuwa Chuo cha Bandari kina mchango muhimu katika kuzalisha wataalamu mahususi wa sekta hiyo, wakiwemo maafisa usafirishaji wa majini (Shipping Officers) na maafisa nyaraka (Documentation Officers).
Amesema kupitia kongamano hilo, wahitimu wamejadili namna ya kutumia utaalamu wao kutoa ushauri kwa Serikali na mamlaka husika kuhusu mbinu za kuongeza tija na ufanisi katika sekta ya bandari na uchukuzi wa majini.
