DAR ES SALAAM
WIZARA ya Maendeleo ya Vijana inatarajia kuwasilisha mafanikio ya mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita, kipindi cha pili, katika sekta ya maendeleo ya vijana kupitia tukio maalum litakalofanyika Novemba 23, mwaka huu, jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Maendeleo ya Vijana), Joel Nanauka, amesema tukio hilo lenye kaulimbiu ya “Mwaka Mmoja, Vijana Pamoja” litafanyika katika ukumbi wa The Super Dome, Masaki, kuanzia saa 2:00 asubuhi.
Akizungumza na waandishi wa habari mapema leo jijini Dar es Salaam, amesema tangu kuanzishwa kwa wizara hiyo Desemba 19, 2025, imeendelea kutekeleza programu mbalimbali zinazolenga kuwawezesha vijana kiuchumi, kuboresha malezi na makuzi, kuimarisha elimu ya uraia na uzalendo pamoja na kuratibu majukwaa ya vijana.
Amesema katika tukio hilo, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anatarajiwa kuwa mgeni rasmi na kuzindua mifumo miwili ya kidijitali itakayoboresha huduma kwa vijana nchini.
Mifumo hiyo ni pamoja na Mfumo wa Uwezeshaji wa Vijana (YES), unaolenga kuwaunganisha vijana na taarifa za huduma na fursa zinazotolewa na Serikali pamoja na wadau mbalimbali.
Ameeleza kuwa mfumo huo tayari umeanza majaribio na zaidi ya vijana 155,000 wamejisajili.
Mfumo mwingine ni wa Uratibu wa Maendeleo ya Vijana, utakaowezesha wizara, taasisi za umma, serikali za mitaa na wadau wengine kushirikiana katika kupanga, kutekeleza na kufuatilia programu za maendeleo ya vijana.
Aidha, tukio hilo litahusisha maonesho ya bidhaa, ubunifu na huduma zinazotolewa na vijana, taasisi za fedha na sekta binafsi, pamoja na ushuhuda wa vijana walionufaika na fursa katika sekta za viwanda, kilimo cha umwagiliaji, uvuvi wa vizimba na zabuni za Serikali.
Maonesho hayo pia yatatoa elimu kuhusu upatikanaji wa mitaji na mikopo, usajili wa biashara, masuala ya kodi, manunuzi ya umma, masoko na matumizi ya teknolojia.
Wizara hiyo imewahimiza vijana, viongozi na wadau wa maendeleo kushiriki katika tukio hilo, ambalo pia litarushwa mubashara kupitia vyombo mbalimbali vya habari.
