Na Mwandishi wetu
MAMLAKA ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imewataka Watanzania kujiunga na Bima ya Afya mapema kabla ya kuugua ili kujihakikishia upatikanaji wa huduma za matibabu na kupunguza mzigo wa gharama za matibabu wanapopata changamoto za kiafya.
Rai hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Kamishna wa Bima ambaye pia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa TIRA, Dkt. Baghayo Abdallah Saqware, wakati akizungumza na wahariri na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa mfumo wa Bima ya Afya kwa wote nchini.
Amesema mfumo huo ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za afya bila kujali hali yake ya kiuchumi, huku TIRA ikiwa na jukumu la kusimamia watoa huduma za Bima ili kuhakikisha wanachama wanapata huduma stahiki bila vikwazo visivyo vya lazima.
Amesema awamu ya kwanza ya mfumo huo ilizinduliwa Oktoba 22, 2026, kwa lengo la kusajili wananchi wasio na uwezo katika mifuko ya Bima ya Afya, huku awamu ya pili ikizinduliwa Oktoba 26, 2026, na Waziri wa Afya kwa ajili ya kuwajumuisha Watanzania wote, wakiwemo wenye uwezo na wasio na uwezo.
Kwa mujibu wa utaratibu huo, Serikali inagharamia bima ya afya kwa wananchi wasio na uwezo, wakati wenye uwezo wanatakiwa kujilipia kupitia kampuni na mifuko mbalimbali ya Bima ya Afya.
Dkt. Saqware amesisitiza umuhimu wa wananchi kuchukua Bima ya Afya wakiwa bado hawajaugua, akieleza kuwa kufanya hivyo kunawasaidia kujikinga na changamoto za kifedha na kuhakikisha wanapata huduma za matibabu wanapozihitaji.
