Na Mwandishi wetu, Geita
Ufugaji wa samaki kwa kutumia teknolojia ya vizimba umeanza kuongeza upatikanaji wa samaki nchini na kupunguza changamoto ya upungufu wa samaki, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Alexander Mnyeti, amesema.
Mnyeti amesema uwekezaji katika teknolojia hiyo ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya kuongeza uzalishaji wa samaki na kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata chakula hicho.
Alitoa kauli hiyo Novemba 20, 2026, wakati wa hafla ya kuwawezesha vijana 85 mitaji kupitia programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora katika sekta ya Uvuvi (BBT-Uvuvi), watakaofuga samaki kwa njia ya vizimba mkoani Geita.
Amesema bila uwekezaji katika ufugaji wa samaki, nchi ingeendelea kukabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa samaki kutokana na kupungua kwa samaki katika baadhi ya maeneo ya maji.
“Kama Mheshimiwa Rais asingefanya hivi, baada ya muda fulani kusingekuwa na samaki wa kula hapa Tanzania kwa sababu maziwa tuliyonayo hayana samaki kwa hivi sasa,” amesema.
Mnyeti pia amekemea taarifa zinazodai kuwa samaki wanaofugwa kwenye vizimba hawana ubora ukilinganisha na wanaovuliwa katika mazingira ya asili. Amesema ufugaji huo unawezesha kufuatilia aina ya chakula wanachopewa samaki, jambo alilolitaja kuwa sehemu ya kuhakikisha ubora wao.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi, Merisia Mparazo, amesema programu ya BBT-Uvuvi inalenga kuwawezesha vijana kupata ujuzi, mitaji na fursa za kujiajiri kupitia shughuli za uzalishaji katika sekta ya uvuvi.
Amesema hatua hiyo inatarajiwa kuongeza kipato cha vijana, kuchangia upatikanaji wa chakula na lishe bora, pamoja na kukuza uchumi wa taifa.
Uwezeshaji huo umefanyika siku chache baada ya baadhi ya wanufaika wa awamu hiyo kuanza kuvuna samaki waliowafuga kwenye vizimba walivyokabidhiwa Machi 7, 2026.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa, samaki waliouzwa kutoka katika vizimba vitatu pekee waliwaingizia wanufaika hao faida ya Sh milioni 76.4.


