Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Mwanamitindo Mtanzania na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wanamitindo Tanzania (TAMOA), Mariam Isack Kissa, anatafuta udhamini wa tiketi ya ndege yenye thamani ya takribani Sh milioni tano ili kushiriki mashindano ya Tisa ya Seychelles Fashion Week, inayotarajiwa kufanyika Cap Lazare Nature reserve, Novemba 25 hadi 30 mwaka huu nchini Seychelles.
Mariam amesema amepata nafasi ya kushiriki maonesho hayo baada ya kuona tangazo lake mtandaoni na kuwasilisha maombi. Kwa mujibu wake, waandaaji wamekubali kugharamia malazi na chakula wakati wa tukio hilo, huku gharama za usafiri wa kwenda na kurudi zikiwa 'mzigo' mkubwa kwake.
Gharama hiyo imekuwa kikwazo cha pekee, huku akiiomba Serikali, Kampuni, wadau wa sekta ya ubunifu na watu binafsi kumsaidia kupata tiketi ili aweze kushiriki na kuiwakilisha Tanzania katika jukwaa hilo la kimataifa.
"Ninapenda sana Uanamitindo. Nimepata nafasi ya kushiriki maonesho haya na waandaaji wamekubali kunigharamia malazi na chakula, lakini usafiri umebaki kuwa jukumu langu. Naomba Serikali na wadau mbalimbali wanisaidie kupata tiketi ya ndege ili niweze kuiwakilisha Tanzania," amesema Mwanamitindo huyo.
Kwa sasa, Hana Menejimenti, na amekuwa akiomba msaada kwa ndugu na jamaa wa karibu, huku sapoti kubwa na ya pekee anayoipata ni kutoka kwa mama yake pekee.
"Mama yangu ananitia moyo sana, na sitarajii kumuangusha. Hata nikifanya chochote kwenye mitindo sifanyi kwa ajili yangu tena. ninafanya kwa sababu ninajua yupo mama ananitazama, na sina budi kufanya kwa bidii zote na nidhamu ya hali ya juu." aliongezea.
Wadau wanaotaka kumuunga mkono wanaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0621 719 379 kwa maelezo zaidi.
Katika masuala ya Mitindo, Mariam alianza safari yake ya kitaaluma ya uanamitindo tangu mwaka 2014 na ameshiriki maonesho mbalimbali ndani na nje ya nchi, huku akijihusisha pia na kuwaendeleza wanamitindo wengine.
"ili ukue ni lazima utegemeane na wengine, ndipo unapofanya kazi, mazoezi, na hata muda ukifika wa kupanda juu, unakuwa na uzoefu wa kutosha ambao mtu yeyote hawezi kuutoa kwako hata iweje" alisisitiza.
Mariam pia ameweza kurekodi nyimbo kadhaa za rap, Hip hop, fani ambayo hajutii kuifahamu huku akiendeleza pia uzoefu alionao katika taaluma ya utafiti na utaalamu wa mipango na maendeleo.
Mpaka anazungumza na Charlii Media, Mariamu amesajiliwa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa kibali halali chenye namba za usajili BST-9684-2026-1726.
Katika jukwaa la kimataifa, ameweza kuiwakilisha Tanzania katika maonesho ya mitindo nchini Guinea, Uganda, Kenya na Afrika Kusini. Mwaka 2023, alichaguliwa kupitia BASATA kuwa mwanamitindo wa kwanza wa kike kuiwakilisha Tanzania katika tamasha la Salon du Textile Africain (SITA), lililofanyika Conakry, Guinea.
Kabla ya hapo, Mwaka 2022 alipendekezwa kuwania tuzo ya Mwanamitindo Bora wa Kike katika Shining Star Awards nchini Afrika Kusini. Baadaye, alitwaa tuzo ya Mwanamitindo Bora wa Afrika Mashariki katika Fashion Explosion Awards nchini Uganda kwa msimu wa 2022/2023.
Pia, mwaka 2022 alishiriki Pwani International Fashion Week and Awards (PIFWA) shindano maarufu la ulimbwende nchini Kenya, akiwa mwanamitindo wa kwanza wa kike kutoka Tanzania kushiriki jukwaa hilo.
Mafanikio yake mengine ni pamoja na kupendekezwa katika tuzo za Volta Fashion Awards nchini Ghana mwaka 2024 na 2026, Zikomo Fashion Awards nchini Zambia kwa msimu wa 2022/2023, African Fashion Designers Awards (AFDA) mwaka 2023 katika kipengele cha African Fashion Model of the Year, pamoja na Africa Fashion Awards nchini Benin katika kipengele cha Revelation Female Model of the Year mwaka 2023.
Katika kazi zake, ameshirikiana na wabunifu wa mavazi kutoka mataifa mbalimbali, wakiwemo Noor Tribe na Marta Zampolini wa Italia, Clavon Leonard wa Marekani, Jonjo Fashion wa Uganda na Fanice1 wa Kenya, pamoja na wabunifu wengine mbalimbali kutoka Madagascar.
Sekta ya uanamitindo nchini imekuwa na changamoto katika uwekezaji ikihusishwa na uhaba wa wafadhili, malipo yasiyolingana na kazi, ukosefu wa mikataba na madai ya upendeleo katika utoaji wa tuzo, n.k.
Serikali na wadau wanapaswa kuitazama sekta hiyo kama sehemu ya uchumi wa ubunifu inayoweza kutoa ajira kwa vijana, kukuza vipaji na kuitangaza Tanzania kimataifa.
Mariam amemshukuru mama yake mzazi kwa kuwa nguzo ya ushauri na msaada katika safari yake ya uanamitindo, akisema mchango wake umemsaidia kuendelea kuwa na imani na taaluma hiyo tangu alipoanza na umri mdogo mpaka kufikia hatua aliyonayo sasa.




