Waandishi wa Habari za kilimo ikolojia kupewa tuzo

Na Mwandishi Wetu.

MKURUGENZI wa Shirika la Islands of Peace (IDP), Ayesiga Buberwa amesema atashirikisha wadau kilimo ikolojia nchini kuandaa tuzo za waandishi bora wa habari hizo.

Ayesega ameyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya hafla ya uzinduzi wa miradi mipya ya Kilimo Endelevu Arusha+ II, ECO-FOOD II na SAFI Project ambayo imefadhiliwa na mashirika kutoka nchini Ubelgiji na Luxembourg

Amesema wanahabari ni watu muhimu sana katika mifumo endelevu ya chakula na hakuna mtu anayepaswa kuachwa pembeni, hivyo ni vema kuangalia namna ya kuwatambua kwa kuwapa tuzo.

"Kwa sasa watu wanasikia kilimo ikolojia kwa kasi kubwa kuliko miaka mitano iliyopita, na ni kwa sababu yenu wanahabari. Katika mradi wa ECO-FOOD tuna kipengele kabisa cha kuwajengea uwezo wanahabari na tunafikiria kuanzisha Tuzo ya Mwandishi Bora wa Kilimo Ikolojia Tanzania ili kutambua mchango wenu kama chachu ya mabadiliko ya sera na mitazamo," amesema.

Mkurugenzi huyo amesema anaamini wadau wenzake wa kupigania na kuhamasisha wataunga mkono wazo hilo ambalo litaongeza hamasa kwa waandishi kiandika habari za kilimo ikolojia.

Ayesiga amesema wakulima nchini wanapaswa kujikita katika kilimo ikolojia na hilo linaweza kufanikiwa kwa waandishi kuandika habari na makala zenye kuonesha faida yake kwa afya ya mlaji, udongo na mazingira.