Dar es Salaam
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imesema imetoa jumla ya Sh trilioni 4.69 kwa wanafunzi wa Kitanzania tangu kuanza kwa Serikali ya Awamu ya Sita, hatua iliyoongeza idadi ya wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia, amesema hayo wakati akiwasilisha mafanikio ya bodi hiyo kwa wahariri wa habari katika kikao kilichoandaliwa chini ya mwamvuli wa vikao vya Msajili wa Hazina na Taasisi zake.
Amesema fedha hizo zimeongezeka kwa karibu Sh trilioni mbili ikilinganishwa na kipindi cha miaka iliyotangulia, huku idadi ya wanufaika ikifikia wanafunzi 1,069,000.
Kwa mwaka wa fedha 2026/2027, HESLB imepanga bajeti ya Sh trilioni 1.06 kwa ajili ya kuwahudumia wanafunzi 375,000. Bajeti hiyo inaakisi ongezeko la uwekezaji katika mikopo ya elimu ya juu ikilinganishwa na kipindi cha awali, ambapo utoaji wa mikopo ulianza kwa Sh bilioni 255.75 kwa wanafunzi 64,575.
Dkt. Kiwia amesema sifa za msingi za mwombaji wa mkopo ni kuwa Mtanzania, kuwasilisha maombi kupitia mifumo ya HESLB na kupata udahili katika taasisi ya elimu ya juu inayotambulika na mamlaka husika.
Ameongeza kuwa matumizi ya teknolojia yamewezesha takribani asilimia 95 ya shughuli za utoaji mikopo kufanyika kidijitali, hatua iliyosaidia kupunguza urasimu na kuongeza uwazi katika utoaji wa huduma. Mifumo hiyo inajumuisha programu ya HESLB na huduma ya mawasiliano ya Chatbot kupitia WhatsApp, zinazowawezesha wanafunzi kupata taarifa na majibu ya maswali yao kwa haraka.
HESLB imesema itaendelea kushirikiana na taasisi za serikali na sekta binafsi kuboresha huduma zake na kuhakikisha vijana wengi zaidi wanapata fursa za elimu ya juu, kwa lengo la kuimarisha rasilimali watu na kuchangia maendeleo ya uchumi wa nchi.




