Dar es Salaam
Mfuko wa uwekezaji wa Zan Timiza Exchange Traded Fund (ETF) umepokea maombi ya uwekezaji yenye thamani ya Sh9.46 bilioni, sawa na asilimia 189.3 ya lengo la awali la Sh5 bilioni.
Akizungumza katika hafla ya kuorodheshwa kwa mfuko huo katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Afisa Mtendaji Mkuu wa Zan Securities Limited, Raphael Masumbuko, amesema wawekezaji wadogo wamechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio hayo, wakijumuisha asilimia 99 ya wawekezaji 3,189 walioshiriki katika toleo la awali.
Masumbuko amesema toleo hilo lilifunguliwa Agosti 17, 2026, na kufungwa Septemba 17, mwaka huo, huku kiwango cha chini cha uwekezaji kikiwa Sh20,000. Ameishukuru CMSA na wadau wengine kwa kuwezesha kuanzishwa kwa bidhaa hiyo na kupanua fursa za uwekezaji kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Usimamizi na Uchunguzi wa Soko kutoka CMSA, Exaut Julius, amesema Zan Timiza ETF ni mfuko wa kwanza wa aina hiyo wenye uwekezaji wa kikanda kuorodheshwa nchini Tanzania, ukiwekeza katika mifuko ya uwekezaji wa pamoja katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Julius amesema asilimia 98 ya wawekezaji ni wa ndani na asilimia mbili ni wa kigeni, akibainisha kuwa kiwango cha chini cha uwekezaji na matumizi ya programu ya Zan Invest App vimeongeza urahisi wa wananchi kupata fursa za uwekezaji.
Naye mwakilishi wa DSE, Emmanuel Nyalali, amesema kuorodheshwa kwa mfuko huo kutapanua bidhaa za uwekezaji sokoni, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kupata elimu kuhusu manufaa na hatari za uwekezaji kabla ya kufanya maamuzi ya kifedha.
Kwa mujibu wa CMSA, ubunifu wa bidhaa za uwekezaji na kuongezeka kwa ushiriki wa wananchi katika soko la mitaji ni miongoni mwa hatua zinazoweza kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
