Serikali yaweka mikakati ya kusimamia wamiliki wa leseni za uchimbaji madini

 

Dodoma.

Serikali imesema itaendelea kuimarisha usimamizi wa wamiliki wa leseni za uchimbaji madini nchini ili kuhakikisha shughuli za uchimbaji zinafuata sheria na kanuni zilizowekwa, zinaleta tija kwa taifa na kuzingatia usalama wa wafanyakazi pamoja na utunzaji wa mazingira.

Kauli hiyo imetolewa Oktoba 30, 2026, Bungeni na Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, wakati akijibu swali la Mbunge wa Kahama Mjini, Benjamini Ngayiwa, aliyetaka kujua mikakati ya Serikali katika kusimamia wamiliki wa leseni za uchimbaji wa dhahabu ili kuwanufaisha wachimbaji wadogo.

Dkt. Kiruswa amesema usimamizi huo unazingatia Sheria ya Madini, Sura ya 123, pamoja na Kanuni za Haki Madini za mwaka 2018, ambazo zinamtaka kila mmiliki wa leseni kutekeleza masharti ya leseni yake, ikiwemo kuanza uzalishaji kwa wakati, kulipa mrabaha, kodi na ada za Serikali, pamoja na kutoa taarifa sahihi za uzalishaji.

Ameongeza kuwa Serikali inatekeleza Kanuni za Ulinzi wa Mazingira kwa Uchimbaji Mdogo za mwaka 2010 kwa kusimamia Mpango wa Ulinzi wa Mazingira (EPP), unaowataka wachimbaji wadogo kurejesha maeneo waliyoyachimba katika hali salama baada ya kumaliza shughuli zao ili kuzuia uharibifu wa ikolojia na vyanzo vya maji.

Kuhusu usalama wa wafanyakazi, amesema Kanuni za Madini kuhusu Usalama, Afya Kazini na Ulinzi wa Mazingira za mwaka 2010 zinawataka wamiliki wa leseni kuweka mifumo ya kuzuia ajali, kulinda afya za wafanyakazi na kuhakikisha mazingira ya kazi yanazingatia vigezo vya usalama.

Dkt. Kiruswa amesema kupitia Tume ya Madini na Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa (RMOs), Serikali itaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara migodini ili kuhakikisha masharti ya leseni yanafuatwa na kuwawajibisha wamiliki watakaobainika kukiuka taratibu zilizowekwa.