TOAM kupanua wigo wa kilimo hai, kuhakikisha mazao salama na masoko yenye tija

MKURUGENZI wa Taasisi Kivuli ya Kilimo Hai Tanzania (TOAM), Bakari Mongo, amesema mradi mpya wa Kuimarisha Kilimo Ikolojia Hai umeanzishwa ili kuwasaidia wakulima kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kuongeza tija na kupata masoko yenye kuzingatia ubora wa mazao.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa mradi huo unaohusisha Wilaya ya Chamwino na Arusha, Mongo alisema Tanzania tayari ina Mkakati wa Taifa wa Kilimo Ikolojia Hai, na kabla ya mkakati huo wadau mbalimbali walikuwa wakitekeleza shughuli zinazolenga kutatua changamoto za mabadiliko ya tabianchi kwa kutumia mbinu za kilimo ikolojia hai.

"Mradi huu ni mchango mmoja wapo kwa kuwasaidia wakulima kuweza kuboresha mbinu na teknolojia ambazo zinalinda mfumo mzima wa uzalishaji kuwa na ustahimilivu katika mabadiliko ya tabianchi, lakini pia kuongeza tija kwa kuwa na masoko mazuri zaidi ambayo yanazingatia ubora," amesema Mongo.

Mongo amesema licha ya juhudi zinazofanywa, uelewa wa jamii kuhusu kilimo hai bado ni mdogo, hasa kwa walaji na wadau wanaohusika kwenye mnyororo mzima wa thamani wa mazao hayo.

"Uelewa bado ni wa hali ya chini hasa kwa walaji na hata wadau wanaohusika na mnyororo mzima wa mazao ya kilimo hai bado wanahitaji kujengewa uwezo ili wapate maarifa sahihi na wajue namna ya kushirikiana kwa karibu zaidi," alisema.

Aliongeza kuwa lengo ni kuwa na uzalishaji wa mazao ambayo ni salama kwa afya ya mlaji na yanayolinda mazingira kwa ajili ya uzalishaji endelevu.

Akieleza kwanini wilaya hizo mbili zimechaguliwa, Mongo amesema rasilimali hazitoshi, hivyo ni lazima kuchagua maeneo ambayo yanaweza kuleta matokeo makubwa kwa muda mfupi na wengine wajifunze.


"Tumechagua Chamwino na Arusha kwa sababu tayari kuna wadau wanaofanya shughuli za kilimo hai huko. Tunataka ku-leverage utaalamu na resources ili tuweze kufikia matokeo makubwa zaidi. Kama tungechagua eneo ambalo hakuna wadau, ingekuwa vigumu kupata matokeo kwa sababu muda wa mradi ni mfupi na rasilimali sio nyingi," amesema.

Amesema mradi utafanya kazi na vikundi vya wakulima vinavyotumia Mfumo Shirikishi wa Kudhibiti Ubora (PGS), ili bidhaa zao zitambulike tofauti na mazao mengine kwa kutumia nembo hiyo.

Akizungumzia idadi ya wakulima wanaotumia kilimo hai, Mongo alisema ni vigumu kutaja namba kamili kwa sababu idadi inaongezeka kila siku, lakini TOAM ina wakulima zaidi ya 10,000 kupitia wanachama wake.

"Tuna wakulima zaidi ya 10,000. Kwa mfano kule Kusini ambao wanazalisha parachichi, wale wenyewe ni wanachama zaidi ya 1,000," amesema.

Amesema matarajio ya mradi ni kuona ongezeko la wakulima wanaotumia mbinu na teknolojia za kilimo hai, kuongezeka kwa uzalishaji, na kuongezeka kwa vikundi vya PGS ambavyo mwisho wa siku vitakuwa na chombo chao cha kuwasemea ngazi ya taifa.