Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe, amewataka watumishi wa umma kuhakikisha uwekezaji unaofanywa na Serikali unaendana na ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi.
Ametoa wito huo Oktoba 24, 2026, wakati wa ziara yake ya kikazi katika Manispaa ya Mpanda, mkoani Katavi, ambapo alikagua miradi ya maendeleo yenye thamani ya shilingi bilioni 26 katika sekta za elu, afya na miundombinu ya barabara.
Miradi iliyokaguliwa ni pamoja na ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wavulana Katavi Boys, barabara za lami kupitia Mradi wa TACTIC, madaraja mawili na Jengo la Watoto Wachanga katika Hospitali ya Manispaa ya Mpanda.
Akizungumza baada ya kukagua jengo hilo la hospitali, Prof. Shemdoe aliwataka watumishi kuzingatia weledi, uzalendo na lugha nzuri wanapowahudumia wagonjwa na wananchi wengine, akisisitiza kuwa huduma bora ni sehemu muhimu ya kuleta manufaa ya uwekezaji wa Serikali.
“Niendelee kuwaomba watumishi wote, na si wa hapa hospitalini pekee, tuendelee kuwasikiliza na kuwahudumia wananchi kwa lugha nzuri. Kumpa mtu tabasamu kwa kumhudumia vizuri ni baraka kwako, lakini akiondoka akiwa ananung’unika, huwezi kupata baraka,” amesema Prof. Shemdoe.
Aidha, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha uwekezaji huo, akieleza kuwa miradi hiyo inalenga kuboresha huduma za elimu, usafiri na usafirishaji pamoja na matibabu kwa wakazi wa Mpanda. Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Mpanda, Charles Philipo, alimshukuru Rais na kumpongeza Prof. Shemdoe kwa utendaji wake, huku akiomba bweni mojawapo la Katavi Boys lipewe jina la waziri huyo, ombi ambalo aliliridhia.
Miradi hiyo ni sehemu ya uwekezaji wa shilingi trilioni 1.4 uliotajwa kuelekezwa mkoani Katavi kwa ajili ya miradi ya maendeleo tangu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aingie madarakani. Kiasi hicho kilitajwa Oktoba 13, 2026, na Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko, wakati wa ziara ya Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi, mkoani humo.




