Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, ameitaka Tume ya Madini kusimamia utekelezaji wa bei elekezi za madini ya ujenzi na viwandani ili kuhakikisha wachimbaji wadogo wanapata malipo yanayostahili na kunufaika na rasilimali wanazozalisha.
Ametoa agizo hilo Oktoba 26, 2026, jijini Dodoma, wakati wa kikao na wadau wa madini ya viwandani kutoka mikoa mbalimbali nchini, akisisitiza kuwa bei elekezi si jambo la hiari, bali ni muhimu katika kulinda maslahi ya wachimbaji na kuimarisha sekta hiyo.
Mavunde amesema wachimbaji wadogo wanapaswa kuunganisha nguvu na mitaji ili kuanzisha viwanda vya uchakataji wa madini, hatua itakayoongeza thamani ya rasilimali hizo, kupanua fursa za ajira na kuongeza mapato. Ameeleza kuwa sekta ya madini ikisimamiwa vizuri inaweza kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongeza manufaa kwa Watanzania.
Kuhusu utafiti wa madini, amesema Serikali imeridhia kutenga asilimia 10 ya mapato yatokanayo na madini kwa ajili ya utafiti, hatua inayolenga kuongeza taarifa kuhusu rasilimali zilizopo nchini na kufungua fursa zaidi za uwekezaji. Pia amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia juhudi za kuimarisha utafiti wa madini.
Katika hatua nyingine, Mavunde amesema Serikali inafanyia kazi changamoto ya wingi wa tozo zinazokwamisha shughuli za wachimbaji wadogo. Ameeleza kuwa Waziri Mkuu amezitaka Wizara ya Madini, Ofisi ya Rais–TAMISEMI na Wizara ya Fedha kukutana ili kupitia tozo hizo na kubaini zinazopaswa kuondolewa ili kuboresha mazingira ya uchimbaji na biashara ya madini.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, amewahimiza wadau kuanzisha vyama vya ushirika ili kuimarisha mitaji na biashara zao. Amesema ushirika unaweza kuwawezesha wachimbaji kuanzisha vituo vya ununuzi wa madini ya ujenzi, kurahisisha upatikanaji wa masoko na kuongeza uwezo wao wa kiuchumi.



