Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania (Red Cross) mkoani Simiyu kimeimarisha maandalizi ya kukabiliana na majanga kwa kuwajengea uwezo wanachama wake ili waweze kuokoa maisha na kutoa huduma kwa wananchi wakati wa dharura.
Mwenyekiti mpya wa chama hicho mkoani humo, Sitta Tuma, amesema hayo wakati wa makabidhiano ya ofisi na mtangulizi wake, Joyce Nyambita, akieleza kuwa wamejiandaa kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za El Niño zinazotarajiwa kunyesha.
Tuma amesema chama hicho kinaendelea kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kupata mafunzo ya kukabiliana na majanga, kutoa huduma za uokoaji na kuelimisha jamii kuhusu hatua za kuchukua kabla, wakati na baada ya majanga.
Amesema maandalizi hayo yanahusisha mafunzo na upatikanaji wa vifaa muhimu ili kuhakikisha wananchi wanapata msaada kwa wakati, huku akiiomba jamii kushirikiana na Red Cross katika juhudi za kuzuia athari za majanga.
Aidha, Tuma amesema uongozi mpya umeanza kuratibu uanzishwaji wa miradi midogomidogo katika ngazi ya wilaya kwa lengo la kuongeza mapato ya chama hicho. Ameeleza kuwa kila halmashauri ya wilaya ina kikosi cha Red Cross kitakachosaidia kufikisha huduma kwa jamii zinazokumbwa na changamoto.
Kwa upande wake, Nyambita amesema mafanikio ya taasisi yanategemea ushirikiano na mwendelezo wa kazi kati ya viongozi, akibainisha kuwa ataendelea kutoa mchango wake kwa kuhamasisha wananchi kujiandaa na majanga. Naye Mwenyekiti wa Tawi la Red Cross Mji wa Zamani, Isaya Mwinule, amesema tawi hilo litaendelea kuimarisha huduma za kwanza katika ngazi ya jamii ili kuwafikia wananchi wanaohitaji msaada.


