TANESCO kuongeza uwezo wa kituo cha dege mara mbili, kigamboni kupata nafuu ya umeme



KIGAMBONI, DAR ES SALAAM

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) linatarajia kuboresha upatikanaji wa umeme kwa wakazi wa Kigamboni, Dar es Salaam, kupitia mradi wa Sh bilioni 17 wa kuongeza uwezo wa Kituo cha Kupokea na Kupoza Umeme cha Dege.

Mradi huo unahusisha ufungaji wa transfoma mpya yenye uwezo wa MVA 120, ambayo tayari imewasili eneo la mradi. Hatua hiyo itaongeza uwezo wa kituo hicho kutoka MVA 60 hadi MVA 120 ili kukidhi mahitaji ya umeme yanayoongezeka kutokana na ukuaji wa makazi na shughuli za kiuchumi.

Akizungumza kwa niaba ya Meneja wa TANESCO Wilaya ya Kimbiji, Mhandisi Lukaluka Kapinga amesema transfoma iliyokuwepo ilikuwa na uwezo wa MVA 60, ambao umekuwa ukikabiliwa na ongezeko la mahitaji ya umeme na kuchangia changamoto za huduma kwa baadhi ya wateja.

Amesema kuongezeka kwa uwezo wa kituo hicho kutasaidia kuboresha huduma kwa wananchi, wafanyabiashara na taasisi zinazotegemea umeme katika shughuli zao za kila siku.

Kwa upande wake, Meneja wa Mradi wa Upanuzi wa Kituo cha Dege, Mhandisi Edward Ngalamika, amesema utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 79.3, huku ufungaji na majaribio ya kiufundi ya transfoma hiyo yakitarajiwa kukamilika Desemba 22, 2026.

Ngalamika amesema kukamilika kwa mradi kutasaidia kuboresha huduma ya umeme kwa wakazi wa Kigamboni. Wakati huo huo, Kapinga amewaomba wananchi kuendelea kuwa wavumilivu wakati kazi za mradi zikiendelea.

#TANESCO #Umeme #Kigamboni #MiundombinuYaUmeme #Dege