EAC yaweka msisitizo maandalizi ya pamoja kukabili El Niño


Nairobi, Kenya

Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimehimizwa kuunganisha nguvu katika kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua kubwa za El Niño zinazotarajiwa kunyesha katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2026.

Hatua zinazopendekezwa ni pamoja na kuimarisha maandalizi dhidi ya mafuriko na maporomoko ya ardhi, kulinda miundombinu ya usafirishaji na kuhakikisha shughuli za biashara pamoja na maisha ya wananchi haziathiriki kwa kiwango kikubwa.

Wito huo umetolewa katika Mkutano wa Dharura wa Wataalamu wa Sekta Mbalimbali kuhusu Maandalizi na Mwitikio wa Kikanda dhidi ya Mvua Zinazotarajiwa za El Niño Kali, unaofanyika Nairobi, Kenya, kuanzia Novemba 4 hadi 6, 2026.

Akifungua mkutano huo, Mratibu wa Mradi wa Pamoja wa Sekta Mbalimbali wa Usalama wa Chakula na Lishe wa Uganda, Julius Twinamatsiko, amesema utabiri unaonesha uwezekano wa mvua kuwa nyingi kuliko wastani wa kawaida, hivyo nchi zinapaswa kuchukua hatua mapema.

Amezitaka nchi hizo kutambua maeneo yenye miundombinu hatarishi, kuweka njia mbadala za usafiri, kuandaa akiba ya chakula na malisho ya mifugo, pamoja na kuimarisha huduma za afya na mifumo ya kufuatilia magonjwa yanayoweza kuongezeka kufuatia mafuriko.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Sekretarieti ya EAC amesema athari za El Niño zinaweza kugusa zaidi ya mazingira na miundombinu, kwa kuwa zina uwezo wa kuhatarisha amani, usalama na maendeleo ya kiuchumi. Amesisitiza umuhimu wa kuunganisha juhudi za nchi wanachama kupitia mpango wa pamoja wa kikanda.

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo wa wataalamu umeongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Brigedia Jenerali Hosea Ndagala. Mkutano huo unalenga kutathmini uwezo wa nchi kukabiliana na athari hizo, kubaini mapungufu na kuweka mfumo wa uratibu utakaosaidia kulinda maisha, huduma muhimu na biashara katika Afrika Mashariki.