Mbowe kuwania uenyekiti Simba?

Na Mwandishi wetu

KUMEKUWA na tetesi za aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, kutarajia kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa Klabu ya Simba.

Taarifa kutoka kwa watu wa karibu na mwanasiasa huyo zinaeleza kuwa anatarajiwa kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo wakati wowote kuanzia sasa, ingawa bado hajatoa tamko rasmi kuthibitisha nia yake hiyo.

Simba inatarajiwa kufanya uchaguzi wa viongozi wake Januari 30, 2027, ikiwa ni sehemu ya mchakato wa kupata viongozi watakaosimamia klabu hiyo katika kipindi kijacho.

Iwapo taarifa hizo zitathibitishwa, Mbowe, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, atakuwa miongoni mwa wanaoweza kuwania nafasi hiyo katika uchaguzi unaotarajiwa kuvuta hisia za wadau wa soka nchini.

Akizungumzia uwezekano huo, Mwenyekiti wa tawi moja la Simba lililopo Kinondoni, ambaye aliomba jina lake lisitajwe, amesema hatua ya Mbowe kuwania nafasi hiyo inaweza kuleta mabadiliko makubwa ndani ya klabu hiyo.

Amesema Mbowe ana uzoefu wa uongozi na uwezo wa kusimamia taasisi kubwa, hivyo anaamini anaweza kutumia uzoefu huo kuisaidia Simba.

"Ni jambo la faraja sana kwetu. Mbowe tunamjua kwa namna alivyoiongoza CHADEMA na mafanikio yake. Tunaamini anaweza pia kuisaidia Simba," amesema.

Ameongeza kuwa Simba inahitaji viongozi wenye uwezo wa kifedha ili kuimarisha shughuli za klabu hiyo.

"Sikufichi kaka, Simba inahitaji watu wenye hela na Mbowe kila mtu anamjua, mambo ya riziki hayampigi chenga," amesema.