Na Mwandishi wetu
Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia nchini Tanzania yameongezeka kutoka asilimia 6.9 mwaka 2021 hadi asilimia 28.6 mwaka 2025, hatua inayotajwa kuwa maendeleo katika utekelezaji wa mkakati wa taifa wa kuhamasisha matumizi ya nishati hiyo.
Waziri wa Nishati, Juma Homera, amesema hayo Novemba 11, 2026, wakati wa mkutano wa kutangaza mafanikio ya mpito wa nishati nchini na matumizi ya nishati safi ya kupikia katika shule na vituo vya afya, uliofanyika Antalya, Türkiye, pembezoni mwa mkutano wa COP31.
Homera amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuongoza juhudi za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, akisema Tanzania imepiga hatua katika ajenda hiyo barani Afrika.
Ili kuongeza kasi ya mabadiliko hayo, Waziri huyo amesema Wizara ya Nishati itaandaa mkakati wa kuwawezesha vijana kubuni na kutengeneza majiko banifu nchini.
Pia, ameitaka TANESCO, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuongeza kasi ya kutoa elimu na kusambaza majiko banifu pamoja na majiko ya umeme.
Tanzania inalenga kufikisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa asilimia 80 ya wananchi ifikapo mwaka 2034, kupitia Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024–2034.
Lengo hilo linahusisha kupanua upatikanaji wa nishati safi na kupunguza utegemezi wa nishati zinazotumika kwa njia zisizo salama kwa afya na mazingira.

