Masauni azitaka NCMC na CRDB kuhakikisha biashara ya kaboni inawanufaisha Watanzania

Na Mwandishi wetu, Antalya

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, (Muungano na Mazingira) Mhandisi Hamad Masauni, amekitaka Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) na Benki ya CRDB kuhakikisha ushirikiano wao unaleta manufaa ya kiuchumi, kijamii na kimazingira kwa Watanzania kupitia biashara ya kaboni.

Mhe. Masauni ameyasema hayo jijini Antalya, Uturuki, wakati wa hafla ya utiaji saini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) kati ya NCMC na CRDB, inayolenga kukuza soko la kaboni nchini na kupanua fursa za uwekezaji wa kijani.

Amesema kuwa biashara ya kaboni inapaswa kwenda zaidi ya uzalishaji na uuzaji wa mikopo ya kaboni kwa kuhakikisha wananchi wanapata ajira, fursa za biashara, teknolojia mpya na kuboresha maisha yao.

Ameeleza kuwa Tanzania imeitambua sekta hiyo kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 kama moja ya maeneo yanayoweza kusaidia kupata fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuvutia uwekezaji unaozingatia utunzaji wa mazingira.

Akizungumzia ushirikiano huo, Masauni amesema NCMC ina jukumu la kuratibu, kufuatilia na kusimamia biashara ya kaboni nchini, wakati CRDB ina uzoefu katika huduma za kifedha na uwekezaji.

Mkurugenzi Mkuu wa NCMC, Bi. Kathryn Kingaraba (kushoto), akiwa pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank, Dkt. Majid Nsekela, baada ya kusaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) inayolenga kukuza soko la kaboni nchini na kuongeza fursa za uwekezaji wa kijani. Ushirikiano huo unatarajiwa kurahisisha upatikanaji wa mitaji kwa miradi ya kaboni na kuhakikisha jamii zinanufaika kupitia ajira, fursa za biashara na uhamishaji wa teknolojia.

Amesema kuwa kuunganisha uwezo wa taasisi hizo kutasaidia kubaini njia bora za kufadhili miradi inayostahili na kurahisisha upatikanaji wa mitaji kwa waandaaji wa miradi ya kaboni.

Waziri Masauni aiitaka CRDB kutafuta njia bunifu za kifedha, ikiwemo mikopo ya vifaa na dhamana, zitakazosaidia utekelezaji wa miradi hiyo kulingana na tathmini ya benki na mahitaji ya waandaji wa miradi.

Hata hivyo, Masauni amesisitiza kuwa ukuaji wa biashara ya kaboni lazima uendane na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira na Kanuni za Usimamizi wa Mazingira (Biashara ya Kaboni) za mwaka 2022, (iliofanyiwa marekebisho mwaka 2023).

Ameonya kuwa kupata fedha za kuendesha mradi siyo kibali cha kuanza utekelezaji, akisisitiza kuwa kila mradi lazima upitie taratibu za kisheria na upate idhini kutoka mamlaka husika.

Pia, amezitaka taasisi hizo kuhakikisha miradi inayotekelezwa inalinda haki za binadamu, inaheshimu jamii zinazozunguka maeneo ya miradi na kuzingatia misingi ya utunzaji wa mazingira.

Amesema Serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya usimamizi na udhibiti wa biashara ya kaboni ili kuhakikisha inatekelezwa kwa uwazi, uwajibikaji na kwa manufaa ya Taifa na wananchi.