Mradi wa umeme wa Mafia kufungua fursa za uchumi Mkuranga

Mkuranga, Pwani

Wananchi wa Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani wanatarajiwa kupata fursa za ajira na kuchochewa kwa shughuli za kiuchumi kupitia mradi wa kusafirisha umeme kwenda Kisiwa cha Mafia kwa njia maalumu inayopita chini ya bahari.

Mradi huo unahusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa kilovoti 33 kutoka Mkuranga hadi Mafia, ikiwa ni sehemu ya mpango mpana wa Serikali wa kuimarisha upatikanaji wa umeme katika visiwa vya Zanzibar na Mafia.

Akizungumza wakati wa semina ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu mradi huo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Mkuranga, Omary Said, amesema utekelezaji wake unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika na kuchochea uzalishaji pamoja na maendeleo ya wananchi.

Amesema Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) inaendelea kupanua huduma ya umeme, huku akiahidi kuwa uongozi wa wilaya utaendelea kushirikiana na shirika hilo kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa ubora na bila vikwazo vinavyoweza kuchelewesha kukamilika kwake.

Kwa upande wake, Mhandisi Joffrey Katoto, akizungumza kwa niaba ya Mratibu wa Mradi, amesema mpango huo una thamani ya dola za Marekani milioni 283 na unajumuisha njia tatu za kusafirisha umeme. Njia hizo ni Mkuranga hadi Mafia yenye kilovoti 33, Tanga hadi Pemba yenye kilovoti 132 na Ununio hadi Unguja yenye kilovoti 220.

Baadhi ya wananchi na viongozi wa vijiji vilivyopo kwenye maeneo yatakayopitiwa na mradi wamesema semina hiyo imewasaidia kufahamu njia zitakazotumika, maeneo yanayoweza kuathiriwa na utekelezaji pamoja na namna ya kushughulikia changamoto zitakazojitokeza.

Semina hiyo ni sehemu ya maandalizi ya mradi, ikilenga kuimarisha ushirikiano kati ya TANESCO, viongozi wa Serikali na wananchi, pamoja na kuwajengea viongozi wa maeneo husika uwezo wa kutatua kwa haraka migogoro inayoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji.