Mwigulu avutiwa na kiwanda cha mabomba ya maji Ludewa


Uwekezaji wa Sh bilioni 1.2 katika kiwanda cha kutengeneza mabomba ya kusambazia maji wilayani Ludewa, mkoani Njombe, umeelezwa kuwa fursa muhimu ya kukuza uzalishaji wa bidhaa za ndani, kuongeza ajira na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi.

Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, ametoa kauli hiyo leo Novemba 14, 2026, baada ya kutembelea kiwanda cha MALC Investment Company Ltd kilichopo Kata ya Mlangali, wilayani humo na kukagua shughuli za uzalishaji.

Amesema amevutiwa na uwekezaji huo na kazi inayofanyika, huku akimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Maiko Lameck Ng’ahala, kwa uamuzi wa kuwekeza katika uzalishaji wa bidhaa zinazohitajika nchini.

Dkt. Mwigulu amesema mabomba yanayozalishwa kiwandani hapo yana soko kubwa kutokana na mahitaji yake katika miradi ya maji inayotekelezwa na Serikali. Ameeleza kuwa baadhi ya miradi iliwahi kukabiliwa na ucheleweshaji kutokana na mabomba kuagizwa kutoka India, hivyo uzalishaji wa ndani unaweza kusaidia kupunguza changamoto hizo.

Amesema uzoefu wa nchi zilizoendelea unaonesha kuwa uchumi wa viwanda na uongezaji thamani wa bidhaa ni njia muhimu ya kukuza uchumi, kuongeza ajira, kupanua wigo wa kodi na kuongeza mapato ya Serikali.

Akitoa taarifa ya kiwanda hicho, Ng’ahala amesema ujenzi ulianza mwanzoni mwa mwaka 2025 na uzalishaji rasmi kuanza Mei 2026. Ameeleza kuwa kiwanda hicho kwa sasa kinazalisha mabomba ya madaraja A na B, yenye ukubwa tofauti kwa matumizi ya kilimo, umwagiliaji na mahitaji mengine.

Amesema mbali na kuongeza upatikanaji wa bidhaa zinazozalishwa nchini, kiwanda hicho kinalenga kuchangia maendeleo ya kiuchumi ya Ludewa na kutoa ajira kwa wananchi, ambapo hadi sasa kimeajiri vijana 30.