Anatalya, Uturuki
Tanzania imeitaka jumuiya ya kimataifa kuweka mifumo ya biashara ya kaboni inayohakikisha nchi na jamii zinazochangia kulinda mazingira zinapata manufaa stahiki kupitia bei zinazozingatia haki na mgawanyo wa mapato ulio wazi.
Wito huo umetolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati akihutubia Mkutano wa 31 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP31) unaofanyika Antalya, Uturuki, Novemba 11, 2026.
Amesema utekelezaji wa Kifungu cha Sita cha Makubaliano ya Paris unapaswa kujenga mifumo ya biashara ya hewa ukaa yenye uwazi katika upangaji wa bei, mgawanyo wa manufaa na ulinzi wa uadilifu wa mazingira.
Rais Samia amesisitiza kuwa mifumo hiyo inapaswa kuhakikisha rasilimali zinazotokana na biashara ya hewa ukaa zinawanufaisha pia wananchi wanaoishi katika maeneo yanayotekeleza shughuli za uhifadhi, sambamba na kuchangia maendeleo ya taifa.
Ameeleza kuwa Tanzania ina fursa za kuzalisha hewa ukaa katika sekta mbalimbali, zikiwemo usafiri, usimamizi wa taka na uzalishaji wa nishati jadidifu kupitia vyanzo vya maji, jotoardhi na upepo.
Ameongeza kuwa misitu ni rasilimali nyingine muhimu katika fursa hizo, akibainisha kuwa Tanzania ina takribani hekta milioni 48.1 za misitu zinazoweza kuchangia katika juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Amesema ni muhimu fursa hizo kuendelezwa kwa kuzingatia uwazi na haki ili kuhakikisha biashara ya hewa ukaa inalinda mazingira na kuleta manufaa yanayogawanywa kwa usawa kati ya taifa na jamii zinazohusika.




