Dar es Salaam.
Tanzania na Zambia zimejadili mikakati ya kupanua ushirikiano katika sekta ya mafuta ili kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa wananchi wa nchi hizo mbili.
Mazungumzo hayo yamefanyika jijini Dar es Salaam Novemba 11, 2026, kati ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi, Dkt. James Mataragio, na ujumbe kutoka Wizara ya Petroli ya Zambia ulioongozwa na Katibu Mkuu, Prof. Ephraim Munshifwa.
Pande hizo mbili zimejadili masuala mbalimbali yenye maslahi ya pamoja katika sekta hiyo, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na kutafuta maeneo mapya ya kufanya kazi kwa pamoja katika sekta ya mafuta.
Tanzania na Zambia zimekuwa na uhusiano wa muda mrefu katika sekta hiyo kupitia Bomba la Mafuta la TAZAMA, ambalo limekuwa sehemu muhimu ya ushirikiano wa nchi hizo. Mazungumzo ya sasa yanaashiria juhudi za kuendeleza uhusiano huo na kupanua ushirikiano katika maeneo mengine.
Ujumbe wa Zambia ulijumuisha wakurugenzi kutoka Ofisi ya Rais, Wizara ya Petroli, Wizara ya Fedha na Wizara ya Sheria. Kwa upande wa Tanzania, kikao hicho kilihudhuriwa na Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu, Kamishna wa Petroli, Godluck Shirima, pamoja na watendaji kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).



