Toleo Jipya la Android 17 (Update) yalenga kubadili matumizi ya simu kupitia akili bandia


Na Charles Mkoka
Google imeingia rasmi kwenye hatua mpya ya ushindani wa teknolojia baada ya kutangaza maboresho makubwa ya mfumo wa Android 17, unaotarajiwa kuifanya simu ya mkononi kuwa “msaidizi binafsi” mwenye uwezo mkubwa wa kutumia akili bandia (AI) kufanya kazi mbalimbali za kila siku.

Maboresho hayo mapya yanaongozwa na mfumo wa Gemini Intelligence, teknolojia ya AI ambayo sasa itaunganishwa moja kwa moja ndani ya Android, hatua inayomaanisha simu inaweza kuelewa mahitaji ya mtumiaji na kufanya baadhi ya kazi bila kuhitaji maelekezo mengi.

Kupitia mfumo huo, mtumiaji ataweza kuitumia simu kupanga ratiba, kujaza taarifa kwenye fomu, kutafuta taarifa ndani ya Gmail, kuandaa oda za manunuzi mtandaoni pamoja na kusaidia shughuli nyingine za kawaida zinazofanywa kila siku kupitia simu.

Katika maboresho hayo, Google imeongeza uwezo wa Gemini kuelewa kinachoonekana kwenye screen ya simu, ikiwemo picha, maandishi au screenshot, jambo linalotarajiwa kubadili namna watu wanavyotafuta taarifa au kutumia huduma mbalimbali mtandaoni.

Kwa mfano, mtumiaji ataweza kuonyesha picha ya bidhaa au sehemu fulani na simu ikaelewa moja kwa moja kinachotafutwa bila kuandika maelezo marefu.

Android 17 pia inaleta maboresho kwenye mawasiliano kati ya vifaa mbalimbali, ambapo kushare mafaili kati ya Android na iPhone kutakuwa rahisi zaidi kupitia QR Code na mfumo mpya wa Quick Share.

Katika eneo la usalama, Google imesema mfumo huo mpya utaongeza uwezo wa simu kugundua simu za utapeli, kuimarisha ulinzi wa taarifa binafsi pamoja na kuongeza usalama dhidi ya wizi wa simu.

Maboresho hayo yanakuja wakati kampuni mbalimbali za teknolojia duniani zikiingia kwenye ushindani mkubwa wa matumizi ya AI kwenye simu za mkononi, huku Google, Apple na Samsung zikiongeza uwekezaji mkubwa kwenye teknolojia hiyo.

Wachambuzi wa teknolojia wanaamini Android 17 inaweza kubadili kabisa namna watu wanavyotumia simu zao katika kazi, biashara, elimu na maisha ya kila siku, hasa kutokana na uwezo wa AI kufanya baadhi ya kazi ambazo hapo awali zilihitaji mtu kufanya mwenyewe.

Google imesema baadhi ya huduma mpya zitaanza kupatikana kwanza kwenye simu za Pixel pamoja na baadhi ya simu mpya za Samsung kabla ya kusambazwa kwa watumiaji wengine duniani kote.

soma hapa