Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania, mwezi Aprili 2026 ilifanya operesheni maalum jijini Dar es Salaam na kufanikiwa kukamata jumla ya lita 66,048 za kemikali bashirifu zilizooingizwa nchini kinyume na taratibu za kisheria.
Kemikali zilizokamatwa ni Cyclohexanone zenye ujazo wa lita 16,048 pamoja na Extra Neutral Alcohol (ENA) zenye ujazo wa lita 50,000. Aidha, magari mawili yaliyohusika katika usafirishaji wa kemikali hizo yanashikiliwa na watuhumiwa wawili wamekamatwa kuhusiana na tukio hilo.
Kutokana na udhibiti wa dawa za kulevya kuimarika duniani, mitandao ya kihalifu imekuwa ikitumia kemikali bashirifu kuzalisha dawa za kulevya katika maabara bubu. Kemikali hizo ni halali kwa matumizi mbalimbali ya viwandani, kitabibu, kilimo, ujenzi, madini pamoja na tafiti za kisayansi, lakini wahalifu huzitumia vibaya kwa kuzichepusha kutoka katika matumizi halali na kuzitumia kutengeneza dawa za kulevya.
Hali hiyo imeongeza changamoto katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya duniani na kuifanya nchi yetu kuendelea kuimarisha mifumo ya udhibiti wa kemikali bashirifu ili kuzuia uchepushwaji wake katika matumizi haramu.
Uchunguzi uliofanyika umebaini kuwa, kemikali aina ya Cyclohexanone ziliingizwa nchini na kampuni ya Kinglion Investment Company LTD kinyume na matakwa ya mifumo ya udhibiti ikiwemo kibali kutoka Mamlaka husika.
Aidha, kemikali aina ya Extra Neutral Alcohol (ENA) zilikuwa zinasafirishwa kwa kutumia magari ya mafuta aina ya Petrol yaliyobandikwa Danger Petroleum 3YE 1203 aina ya Scania kwa kutumia vibali vya kughushi. Magari hayo yalikuwa yakibeba kemikali kutoka kampuni ya Maranile Group Company Limited iliyopo Kibaha Mkoani Pwani.
Katika operesheni hiyo, Mamlaka ilimkamata Bakira Abel Zacharia (44), mkazi wa Dar es Salaam, dereva wa gari namba T 794 BMB lenye tela tanki namba T 166 AHW lililokuwa limebeba lita 3,000 za kemikali hizo.
Pia, ilikamatwa Vicent Stephen Rashid (26), dereva wa gari namba T 568 EQF lenye tela tanki namba T 640 EQN lililokuwa limebeba lita 20,000 za kemikali hizo.
Majorio ya uingizaji na usafirishaji wa kemikali hizo yanashirifu upeo wa nia ovu ya kuzichepusha kwa matumizi haramu, ikiwemo utengenezaji wa dawa za kulevya. Kemikali aina ya Cyclohexanone ni miongoni mwa kemikali zilizoidhinishwa kimataifa kutumika kutengeneza kutafisha katika maabara bubu zinazozalisha dawa za kulevya aina ya Phencyclidine (PCP).
Aidha, Lita 16,048 za kemikali za Cyclohexanone zilizokamatwa kama zingechapushwa zingeweza kuzalisha Tani 11.4 za dawa za kulevya aina ya Phencyclidine kwa kuwa kilo moja ya kemikali hizo huweza kuzalisha takriban gramu 750 za dawa za kulevya.
Kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali za Viwandani na Majumbani sura 182, usafirishaji wa kemikali umetakiwa taratibu maalumu ikiwemo vibali vya kuingiza na kusafirisha kemikali. Matumizi ya vibali vya kughushi pamoja na utoaji wa taarifa za uongo kuhusu matumizi yaliyokusudiwa ya kemikali husika ni kosa kisheria.
Aidha, usafirishaji wa kemikali kwa njia fiche hususani kwa kutumia magari ya kubeba Petrol ni ukiukwaji mkubwa wa taratibu za udhibiti wa kemikali na ni kiashiria cha uwepo wa jaribio la kuzichepusha kwa matumizi haramu ikiwemo utengenezaji wa dawa za kulevya.
Sambamba na operesheni hiyo, Mamlaka ilifanya operesheni nyingine katika mikoa ya Dodoma, Mtwara, Njombe, Ruvuma, Kilimanjaro, Arusha, Dar es Salaam, Morogoro na Mwanza ambapo jumla ya tani 5.733 za bangi, tani 1.67 za mirungi, gramu 48.23 za heroin pamoja na gramu 113.35 za cocaine zilikamatwa. Aidha, ekari 38.5 za mashamba ya bangi ziliteketezwa na magunia manne pamoja na pikipiki 14 zilizohusishwa na biashara hiyo haramu zilikamatwa. Jumla ya watuhumiwa 84 walikamatwa kuhusiana na ukamataji huo.
Mamlaka itaendelea kushirikiana na taasisi za kitaifa na kimataifa kuimarisha udhibiti wa kemikali bashirifu zinazoweza kutumika katika utengenezaji wa dawa za kulevya.
Hivyo, tunatoa wito kwa wadau wote wa kemikali kuzingatia sheria kanuni na taratibu zilizowekwa pamoja na kutoa ushirikiano kwa vyombo vya udhibiti ili kulinda usalama wa jamii na uchumi wa nchi yetu. Kinyume na hapo, hatua kali za kisheria zitaendelea kuchukuliwa dhidi ya wote watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo.
Mamlaka inawahimiza wananchi kuendelea kutoa taarifa za vitendo vinavyohusiana na dawa za kulevya pamoja na uchepushaji wa kemikali bashirifu ili kusaidia juhudi za Serikali katika mapambano dhidi ya biashara na matumizi ya dawa za kulevya.


