Wafanyabiashara wa madini kutoka ndani na nje ya Tanzania pamoja na wanunuzi wa kimataifa wanatarajiwa kushiriki katika Mnada wa Vito vya Madini Tanzania utakaofanyika Mirerani mkoani Manyara kuanzia Mei 18 hadi 21, 2026.
Mnada huo umeandaliwa na Kituo cha Biashara ya Madini Tanzania (TEC) kwa kushirikiana na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), ukiwa sehemu ya juhudi za Serikali kuimarisha biashara rasmi ya madini na kuongeza ushindani wa Tanzania katika soko la kimataifa la vito vya thamani.
Kwa mujibu wa taarifa ya waandaaji, usajili wa wanunuzi ulianza rasmi Mei 4, 2026 ambapo wanunuzi wa ndani na nje ya nchi wanatakiwa kujisajili kupitia ofisi za Wakala wa Madini zilizopo Arusha na Mirerani kabla ya kushiriki katika mnada huo.
Mnada huo utafanyika katika jengo la TEC lililopo Mirerani, eneo linalofahamika duniani kwa uzalishaji wa madini ya Tanzanite ambayo hupatikana Tanzania pekee.
Tukio hilo linafanyika wakati Serikali ikiendelea na mkakati wa kuifanya Mirerani kuwa kitovu kikubwa cha biashara ya vito vya madini Afrika kupitia ujenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Biashara ya Tanzanite (TEC), ambacho Serikali imesema kipo katika hatua za mwisho kukamilika.
Hatua hiyo inalenga kuongeza uwazi katika biashara ya madini, kupunguza utoroshaji pamoja na kuongeza thamani ya madini yanayozalishwa nchini kabla ya kuuzwa katika masoko ya dunia.
Ripoti mbalimbali zimeonyesha kuwa licha ya Tanzania kuwa nchi pekee inayozalisha Tanzanite, sehemu kubwa ya thamani ya biashara hiyo bado hunufaisha masoko ya nje kutokana na uchakataji na uongezaji thamani kufanyika nje ya nchi.
Wadau wa sekta ya madini wanaamini kuwa mnada huo utafungua fursa zaidi kwa wafanyabiashara wa ndani kupata wanunuzi wa kimataifa huku ukiimarisha ushindani wa vito vya Tanzania katika soko la dunia.
Aidha, ongezeko la mahitaji ya madini ya Tanzanite katika soko la kimataifa linaendelea kuifanya Tanzania kuwa moja ya maeneo muhimu katika biashara ya vito vya thamani duniani.