Serikali yaitaka Mantra kuanza uzalishaji wa Uranium kwa wakati

 
Na Mwandishi wetu

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, ameitaka Kampuni ya Mantra Tanzania Limited kuhakikisha inaanza uzalishaji wa madini ya uranium kwa wakati ili Watanzania waweze kunufaika na fursa za kiuchumi zinazotarajiwa kutokana na utekelezaji wa mradi mkubwa wa Mkuju River uliopo Namtumbo mkoani Ruvuma.

Dkt. Kiruswa ametoa kauli hiyo Mei 13, 2026 jijini Dodoma alipokutana na viongozi wa kampuni hiyo kujadili maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati.

Alikumbusha kuwa mwezi Julai mwaka 2025, Rais Samia Suluhu Hassan alizindua kiwanda cha majaribio cha kusindika uranium cha Mantra Tanzania, hatua iliyolenga kujaribu teknolojia ya usindikaji pamoja na kukusanya taarifa muhimu kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda kikubwa cha uzalishaji.

Dkt. Kiruswa alisema Serikali haina mpango wa kufuta leseni kubwa ya uchimbaji iliyotolewa kwa kampuni hiyo, huku akiitaka kuongeza kasi ya kutafuta mtaji ili shughuli za uzalishaji zianze kwa wakati uliopangwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Ilya Shchukin, alisema kampuni ipo katika hatua za mwisho za kutafuta fedha za kuanza ujenzi wa mgodi pamoja na kiwanda kikubwa cha usindikaji wa uranium.

Alisema kampuni inaendelea na mazungumzo na taasisi mbalimbali za kifedha kutoka Urusi pamoja na benki za Tanzania ikiwemo CRDB Bank Plc na NMB Bank Plc ili kufanikisha upatikanaji wa mtaji wa mradi huo.

Hata hivyo, alisema changamoto kubwa inayochelewesha baadhi ya maamuzi ya kifedha ni muda uliobaki wa leseni ya uchimbaji ambayo inatarajiwa kuisha Aprili mwaka 2028, jambo linalofanya baadhi ya taasisi za fedha kuwa na tahadhari katika utoaji wa mikopo ya muda mrefu.

Kwa mujibu wa kampuni hiyo, mradi wa Mkuju River unatarajiwa kuzalisha zaidi ya ajira 4,000 za moja kwa moja kwa wakazi wa Namtumbo na maeneo jirani, huku zaidi ya kaya 21,000 zikitarajiwa kunufaika kupitia shughuli mbalimbali za kiuchumi zitakazochochewa na mradi huo.

Katika eneo la uwajibikaji kwa jamii, kampuni hiyo imesema imeendelea kuwekeza katika sekta za elimu, afya, mazingira, miundombinu pamoja na uwezeshaji wa vijana na wanawake wanaoishi maeneo yanayozunguka mradi huo.

Naye Meneja wa Mahusiano na Jamii Endelevu wa kampuni hiyo, Majani Wambura, ameiomba Tume ya Madini kuihuisha leseni ya kampuni ili kuongeza uwezekano wa kupata mikopo kutoka taasisi za fedha kwa urahisi zaidi.

Kwa mujibu wa kampuni hiyo, Mradi wa Mkuju River unatarajiwa kuzalisha takribani tani 3,000 za uranium kwa mwaka pindi utakapoanza rasmi uzalishaji, hatua inayotarajiwa kuiweka Tanzania miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa uranium barani Afrika.

Mantra Tanzania Limited ni kampuni tanzu ya Uranium One Group, sehemu ya sekta ya nyuklia ya Urusi inayosimamia mradi huo mkubwa wa uchimbaji na usindikaji wa uranium nchini Tanzania.