Ugunduzi wa jiwe kubwa la ruby lenye uzito wa takribani karati 11,000 nchini Myanmar umeibua msisimko mkubwa katika sekta ya madini ya vito duniani huku wachimbaji, wafanyabiashara na wataalamu wa madini wakilitaja kuwa moja ya mawe makubwa zaidi kuwahi kupatikana katika miaka ya karibuni.
Jiwe hilo linaripotiwa kugunduliwa katika eneo la Mogok, jimbo ambalo kwa miongo mingi limekuwa likifahamika kimataifa kama moja ya maeneo yenye ruby bora zaidi duniani.
Myanmar imeendelea kushikilia nafasi muhimu katika soko la vito vya thamani kutokana na ubora wa ruby zake maarufu kwa rangi nyekundu yenye thamani kubwa katika masoko ya kimataifa.
Wataalamu wa sekta ya vito wanasema ukubwa wa jiwe hilo unaweza kulifanya kuwa miongoni mwa mawe yenye thamani kubwa zaidi kuwahi kupatikana iwapo vipimo vya ubora wake vitathibitishwa rasmi.
Picha na video za jiwe hilo tayari zimeanza kusambaa katika mitandao ya kijamii na majukwaa ya biashara ya madini, huku zikivutia maelfu ya watu duniani.
Mogok, eneo ambalo ruby hilo limepatikana, limekuwa likijulikana kwa kuzalisha vito vya thamani kwa zaidi ya karne moja na mara nyingi huitwa “Valley of Rubies” kutokana na historia yake katika biashara ya madini hayo.
Sekta ya madini ya Myanmar imeendelea kuvutia wawekezaji wa kimataifa licha ya changamoto za kisiasa na kiusalama zinazoikabili nchi hiyo katika miaka ya hivi karibuni.
Ugunduzi huo umeongeza tena mjadala kuhusu utajiri mkubwa wa madini uliopo katika bara la Asia pamoja na ushindani mkubwa unaoendelea katika soko la vito vya thamani duniani.
Wachambuzi wa biashara ya madini wanasema mahitaji ya ruby yanaendelea kuongezeka katika masoko ya kifahari duniani, hususan Asia, Mashariki ya Kati, Ulaya na Marekani, ambako mawe makubwa na yenye ubora wa juu huuza kwa mamilioni ya dola.
Kwa sasa, mamlaka pamoja na wataalamu wa madini nchini Myanmar wanatarajiwa kufanya tathmini rasmi ya ubora, thamani na kiwango halisi cha jiwe hilo kabla ya hatua nyingine za biashara au maonesho ya kimataifa kuanza.