Kijana afikishwa mahakamani kwa kulamba mirija ya juice


Na Mwandishi wetu

Kijana mmoja raia wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 18 amefikishwa mahakamani nchini Singapore baada ya video kusambaa mtandaoni ikimuonyesha akilamba mirija ya vinywaji kwenye mashine ya kuuza juice.

Kijana huyo anayeitwa Didier Gaspard Owen Maximilien anakabiliwa na mashitaka ya kufanya uharibifu pamoja na kusababisha usumbufu kwa umma.

Kwa mujibu wa mamlaka za Singapore, tukio hilo lilitokea Machi 12 mwaka huu katika eneo la Goldhill Centre, Thomson Road.

Kampuni ya iJooz inayomiliki mashine hiyo ililazimika kubadilisha mirija yote 500 iliyokuwa ndani ya mashine pamoja na kufanya usafi maalum wa mashine hizo baada ya video kusambaa.

Waendesha mashitaka walidai kijana huyo alijirekodi akifanya kitendo hicho, kisha akaweka video hiyo kwenye Snapchat kabla ya kuisambaza kupitia Instagram Story.

Tukio hilo lilizua mjadala mkubwa mtandaoni huku wananchi wengi wakikosoa tabia ya kufanya vitendo vya hatari kwa ajili ya kutafuta umaarufu kwenye mitandao ya kijamii.

“Kutafuta views hakupaswi kuhatarisha afya za watu wengine,” mmoja wa watumiaji wa mtandao wa X aliandika.

Kampuni ya iJooz ilisema ilitoa taarifa polisi mara baada ya kuona video hiyo na kuongeza ukaguzi pamoja na hatua za usafi kwenye mashine zake.

Shule anayosoma kijana huyo, ESSEC Business School, nayo ilisema imeanza uchunguzi wa ndani kuhusu tukio hilo.

Mahakamani, mawakili wa Maximilien waliieleza mahakama kuwa kijana huyo anaishi Singapore peke yake kwa ajili ya masomo na mzazi wake alikuwa anatarajiwa kusafiri kwenda nchini humo.

Mahakama ilimruhusu dhamana ya dola za Singapore 5,000 huku kesi hiyo ikiahirishwa hadi Mei 22 mwaka huu.

Iwapo atapatikana na hatia ya kufanya uharibifu, anaweza kufungwa hadi miaka miwili, kutozwa faini au vyote kwa pamoja.

Kwa kosa la kusababisha usumbufu kwa umma, sheria za Singapore zinaeleza anaweza kufungwa hadi miezi mitatu au kutozwa faini.