Benki ya Dunia kuisaidia NEMC kujijenga kimamlaka kwenye mazingira


Na Mwandishi wetu 

Benki ya Dunia imeeleza kuridhishwa na maendeleo ya Tanzania katika usimamizi wa mazingira na kuahidi kuendelea kushirikiana na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) katika kuimarisha mifumo ya usimamizi wa mazingira nchini.

Hatua hiyo imeelezwa katika kikao kati ya ujumbe wa Benki ya Dunia ulioongozwa na Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Bi Anna Wellenstein pamoja na Bw. Muhammad Kandeel, na viongozi wa NEMC wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu Dkt. Immaculata Semesi.

Majadiliano hayo yalihusu namna ya kuimarisha utekelezaji wa tathmini za athari kwa mazingira, kujenga uwezo wa wataalamu wa mazingira na maafisa wa serikali pamoja na kuwajengea wadau uwezo wa kutumia mifumo na taratibu za Benki ya Dunia katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Katika kikao hicho, NEMC ilishukuru Benki ya Dunia kwa ushirikiano wake katika utekelezaji wa Mradi wa Kudhibiti Matumizi ya Zebaki kwa Wachimbaji Wadogo (EHPMP), ambao umesaidia kupunguza matumizi ya zebaki na kuimarisha usimamizi wa kemikali katika shughuli za uchimbaji mdogo wa dhahabu nchini.

Kwa upande wake, Benki ya Dunia ilieleza kufurahishwa na mafanikio ya mradi huo na kuahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kuimarisha mifumo ya usimamizi wa mazingira na utekelezaji wa sheria za mazingira.

Kikao hicho kinakuja wakati NEMC ikielekea kutimiza miaka 40 tangu kuanzishwa kwake, huku serikali ikiendelea kuimarisha taasisi hiyo kama sehemu ya mkakati wa taifa wa hifadhi ya mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.