Na Mwandishi wetu
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ametembelea ujenzi wa viwanja vya Farasi na Leaders Club wilayani Kinondoni na kuagiza mkandarasi kuhakikisha kazi zinakamilika kwa wakati kuelekea mashindano ya AFCON.
Viwanja hivyo ni miongoni mwa maeneo yatakayotumika kwa mazoezi wakati wa mashindano hayo yatakayofanyika Tanzania.
Akiwa katika ziara hiyo, Chalamila amesema AFCON inapaswa kuwa fursa ya kiuchumi kwa wananchi wa Dar es Salaam.
Ameitaka Halmashauri ya Kinondoni kutumia mashindano hayo kukuza utalii, biashara ndogo ndogo pamoja na shughuli nyingine zitakazowaongezea wananchi kipato.
Pia ameagiza kufanyika maboresho ya maeneo ya fukwe ikiwemo Coco Beach ili kuvutia wageni watakaokuja wakati wa mashindano hayo.
Chalamila amesema maeneo hayo yanaweza kusaidia kutangaza utalii wa vyakula vya Kitanzania pamoja na tamaduni za nchi.
“Halmashauri iweke mazingira mazuri kwa wananchi kufanya biashara zao wakati wa AFCON,” amesema.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kukamilika kwa miradi hiyo kwa wakati ili kuendelea kuilinda heshima ya Tanzania kimataifa.
Amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameendelea kuipa Tanzania heshima kubwa kwa kuwa mwenyeji wa mashindano hayo makubwa ya Afrika.
Katika ziara hiyo pia, Chalamila ameagiza kuboreshwa kwa miundombinu ya barabara, huduma za maji pamoja na mifumo ya ulinzi na usalama kwenye maeneo yanayozunguka viwanja hivyo.
Amesema taa za barabarani na usafi wa mazingira vinapaswa kupewa kipaumbele kabla ya mashindano hayo kuanza.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, amesema maboresho ya viwanja hivyo hayatazuia wananchi kuendelea kuvitumia kwa shughuli mbalimbali za kijamii.
Amesema shughuli za mazoezi na mbio za mwendapole zimekuwa muhimu katika kusaidia wananchi kupambana na magonjwa yasiyoambukiza kama shinikizo la damu na kisukari.
soma

