Wizara ya Madini imetoa siku tatu kwa wachimbaji na wanunuzi wa madini ya jasi kuwasilisha mchanganuo wa gharama za uzalishaji ili kusaidia Serikali kupata suluhisho la mgogoro wa bei ya madini hayo.
Agizo hilo limetolewa Mei 14, 2026 jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, wakati wa kikao kati ya wachimbaji wa jasi na wanunuzi wakiwemo kampuni za saruji.
Dkt. Kiruswa amesema Serikali inataka kupata picha halisi ya changamoto zinazokabili kila upande kabla ya kufikia maamuzi.
“Tunataka kila upande ueleze changamoto zake ili tupate suluhisho ambalo litawanufaisha wote,” amesema.
Pia amesema Serikali itafuatilia malalamiko kuhusu baadhi ya tozo zinazodaiwa kuongeza gharama za uzalishaji wa jasi.
Kwa upande wao, wachimbaji wamesema gharama za uzalishaji zimeongezeka kwa miaka ya karibuni huku bei ya jasi ikibaki ileile tangu mwaka 2016.
Mwenyekiti wa Wachimbaji Wadogo wa Madini ya Jasi Mkoa wa Lindi, Salum Kassim, amesema kupanda kwa bei ya mafuta, vipuri vya mitambo na mishahara ya wafanyakazi kumeathiri biashara hiyo.
Amesema hali hiyo imefanya baadhi ya wachimbaji kushindwa kupata faida.
Kutokana na hali hiyo, wachimbaji wamependekeza bei ya tani moja ya jasi kwa Dar es Salaam na Pwani iongezwe kutoka Tshs 110,000 hadi Tshs 150,000.
Kwa Mkoa wa Mtwara, wamependekeza bei iongezeke kutoka Tshs 75,000 hadi Tshs 95,000 kwa tani.
Mkuranga bei imependekezwa kupanda kutoka Tshs 95,000 hadi Tshs 130,000, huku Kiranjeranje ikipendekezwa kutoka Tshs 60,000 hadi Tshs 75,000 kwa tani.
Hata hivyo, kampuni za saruji zimeonyesha wasiwasi kuhusu ongezeko hilo.
Mkurugenzi wa Manunuzi wa Dangote Cement, Halima Kuchwa, amesema kupanda kwa gharama za jasi kunaweza kuongeza gharama za uzalishaji wa saruji na hatimaye bei kwa wananchi.
“Gharama zikiongezeka upande wa malighafi, zinaweza kumuathiri pia mtumiaji wa mwisho,” amesema.
Baadhi ya wadau wa sekta ya ujenzi wanasema Serikali inapaswa kupata uwiano ambao utawasaidia wachimbaji kuendelea na uzalishaji bila kuongeza mzigo mkubwa kwa watumiaji wa saruji.
Madini ya jasi hutumika kutengeneza saruji, gypsum na bidhaa nyingine za ujenzi.
Maeneo makubwa ya uzalishaji nchini ni pamoja na Lindi, Mtwara, Pwani na Mkuranga