Dkt. Mwinyi Aipongeza UVCCM Kwa Kuipa CCM Ushindi Mkubwa Uchaguzi Mkuu 2025

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amepongeza Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) kwa kazi kubwa na ya kujitolea waliyoifanya wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2025 na kukipatia ushindi mkubwa Chama Cha Mapinduzi.

Dkt. Mwinyi ametoa pongezi hizo leo tarehe 16 Mei 2026, alipojumuika na vijana wa CCM katika sherehe ya “DKT. MWINYI UVCCM USHINDI PARTY” iliyofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Vijana wa CCM Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja.

Katika hafla hiyo, Dkt. Mwinyi amewahakikishia vijana kuwa Serikali itatekeleza kwa umakini mkubwa ahadi zote zilizotolewa wakati wa kampeni ili kuwawezesha vijana kiuchumi na kijamii, huku akiutaka uongozi wa UVCCM kujipanga vizuri kwa ajili ya utekelezaji wa mipango hiyo

Aidha, ameyapongeza makundi yote ya hamasa kwa kutekeleza majukumu yao kwa uzalendo, nidhamu na ufanisi mkubwa katika kukitumikia Chama Cha Mapinduzi wakati wa kampeni za uchaguzi.

Amesema CCM kinajivunia kuwa na vijana wenye ari ya kujitolea kwa ajili ya chama chao na Taifa kwa ujumla.

Hafla hiyo ilijumuisha dhifa ya chakula cha mchana pamoja na burudani mbalimbali zikiwemo muziki wa kizazi kipya, taarabu, ngoma za asili na sanaa za utamaduni.

Sherehe hiyo imefanyika kufuatia ahadi aliyoitoa Dkt. Mwinyi wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 kwa makundi ya hamasa ya vijana wa CCM kutokana na mchango wao mkubwa wa kukipatia ushindi wa kishindo Chama Cha Mapinduzi.

Soma