Prof. Shemdoe ametoa wito huo leo Mei 16, 2026 Jijini Baku nchini Azerbaijan wakati ujumbe wa Tanzania ulioongozwa na Waziri wa Ardhi Mhe. Dr. Leonard Akwilapo ulipokutana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Makazi yaani UN-HABITAT katika kikao kazi ambacho ni sehemu ya Mkutano Mkubwa wa kidunia wa maswala ya Miji (World Urban Forum).
"Ni vyema kwa kushirikiana na UN HABITAT, tukajitahidi kuandaa na kuimarisha upangaji wa miji inayoibukia hasa kwenye vituo vikuu vya treni ya SGR na kuweka pia kongani za kilimo ambazo zitazalisha kwa ajili ya treni ya mizigo kusafirisha mazao ya kilimo na aina yeyote ya mazao yatakayozalishwa kwenye maeneo hayo," amesisitiza Prof. Shemdoe.
Aidha, Prof. Shemdoe amesema Serikali inayoongozwa na Dkt.Samia Suluhu Hassan inaendelea na mpango wa kuimarisha mji wa kibiashara wa Kwala kuwa mji wenye tija ili kuipunguzia Dar es Slaam msongamano, hivyo ameiomba UN HABITAT kushirikiana na Wizara ya Ardhi pamoja na OWM TAMISEMI kuikaribisha Sekta Binafsi kufanya uwekezaji katika eneo hilo kwa kuzingatia mipango miji na taratibu zake.Mambo mengine yaliyojadiliwa kwenye kikao hicho ni pamoja na uzinduzi wa ofisi za UN HABITAT Dodoma, uandaaji wa Mkutano mkubwa wa Africa Urban Forum na masuala ya mashirikiano ya karibu kati ya Tanzania na UN-HABITAT.

