iPhone 18 huenda ikauzwa bei zaidi Tanzania

Na Mwandishi wetu

Kampuni ya teknolojia ya Apple inapanga kuzindua simu zake mpya za iPhone 18, kwa gharama ya juu zaidi.

Kwa mujibu wa ripoti za teknolojia zilizochapishwa na Forbes pamoja na wachambuzi wa soko la simu duniani, Apple huenda ikazindua kwanza matoleo ya 'bei mbaya' ya iPhone 18 Pro na Pro Max mwaka huu, huku simu za kawaida (plain na Air) zikisubirishwa hadi mwakani (2027).

Ripoti hizo pia zinaeleza kuwa Apple inaweza kuongeza bei za baadhi ya simu zake kutokana na gharama za uzalishaji kuongezeka pamoja na ushindani wa teknolojia mpya za akili unde (AI).

Hatua hiyo inaweza kupelekea gharama za iPhone kuwa kubwa zaidi sokoni, hadi kwa matoleo ya zamani. 

Katika maduka mengi ya simu jijini Dar es Salaam, Arusha na Mwanza, baadhi ya iPhone mpya huuzwa kati ya Tshs milioni 3 hadi 5 ikitegemeana na aina ya simu na ukubwa/uwezo wake.

Tofauti na Marekani na Ulaya, wateja wengi hununua simu kwa mikataba ya kampuni za simu, hata nchini, Watanzania wengi hununua iPhone kwa fedha taslimu au kupitia soko la simu zilizotumika (ku-top up).

Hali hiyo huenda ikapelekea ongezeko lolote la bei duniani, kuonekana moja kwa moja kwenye soko letu la ndani.

Wachambuzi mbalimbali wa teknolojia wanasema kuwa Apple sasa inaonekana kulenga zaidi wateja wa premium wanaotaka simu za Pro.

Kampuni hiyo pia inatajwa kuendelea na maandalizi ya simu inayokunjika (Foldable), ili kushindana na Samsung na kampuni nyingine.

Kwa miaka ya karibuni, vijana wengi Tanzania wamekuwa wakitumia iPhone kwa ajili ya biashara mtandaoni, kupiga picha, kurekodi video pamoja na kutengeneza maudhui ya mitandaoni, huku wengine wakidaiwa kuitumia kama alama ya ufahari.

Pamoja na umaarufu wote huo, bado simu za Android kutoka Samsung, Xiaomi, Tecno na Infinix bado zinaendelea kutawala soko la Afrika na maeneo mengine kutokana na bei nafuu, kupatikana kwa urahisi pamoja na urekebishaji (maintenance).

Apple bado haijaweka wazi, ila taarifa zinasambaa dunia nzima kuhusu mabadiliko haya mapya kwenye  iPhone 18, huku mijadala ikizidi kupamba moto duniani kote