Mchezaji wa zamani wa Timu ya Taifa ya Uingereza na klabu ya Manchester United, Rio Ferdinand, anatarajiwa kuwasili nchini Tanzania wiki ijayo kwa ziara maalum iliyoandaliwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda.Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa, Ferdinand ambaye kwa sasa anafanya kazi ya uchambuzi na utangazaji wa masuala ya michezo, atakuwa na ratiba mbalimbali za kikazi na kijamii akiwa nchini. Miongoni mwa shughuli hizo ni kufanya mazungumzo na Waziri Makonda kuhusu maendeleo ya michezo, hususan soka, pamoja na namna ya kuendeleza ushirikiano wa kimataifa katika sekta ya michezo na utalii.
Mbali na hilo, nyota huyo wa zamani wa soka anatarajiwa kutembelea Bunge la Tanzania na kupata fursa ya kujionea shughuli mbalimbali za kiserikali pamoja na mfumo wa uendeshaji wa shughuli za kibunge nchini.
Katika ziara hiyo pia, Ferdinand anatarajiwa kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ambapo masuala ya michezo, uwekezaji na utalii yanatarajiwa kujadiliwa.
Aidha, Ferdinand atapata nafasi ya kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini Tanzania ikiwa ni sehemu ya kuendelea kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia watu mashuhuri wa michezo. Ziara yake inaelezwa kuwa sehemu ya juhudi za Serikali katika kutumia michezo kama nyenzo ya kukuza diplomasia, utalii na fursa za kiuchumi.
Ujio wa Ferdinand nchini unatarajiwa kuvutia wadau wengi wa michezo pamoja na mashabiki wa soka, hasa kutokana na historia yake kubwa akiwa mmoja wa mabeki bora waliowahi kucheza katika ligi kuu ya England na klabu ya Manchester United.