Huduma ya tiba asilia ya udungwaji wa nyuki maarufu kama Apitherapy imeendelea kuvutia watu wengi kwenye banda la Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika maonesho ya Wizara ya Maliasili na Utalii yanayoendelea mjini Dodoma.
Viongozi, wabunge na wananchi wanaotembelea banda hilo wamekuwa wakipata elimu kuhusu matumizi ya sumu ya nyuki kwenye tiba za asili, huku baadhi yao wakiamua kupata huduma hiyo papo hapo.
Huduma hiyo hutumia sumu ya nyuki kusaidia kupunguza baadhi ya matatizo ya kiafya pamoja na kuimarisha kinga ya mwili.
Katika tiba hiyo, nyuki huwekwa kwenye maeneo maalum ya mwili ili kumdunga mhudumiwa kwa muda mfupi chini ya uangalizi wa wataalamu.
Akizungumza kwenye maonesho hayo, Mhifadhi wa TFS na Afisa Nyuki kutoka Hifadhi ya Mazingira Asilia Vikindu, Brenda Mwakipesile, amesema tiba hiyo imekuwa ikitumika kusaidia watu wenye maumivu ya viungo, arthritis, rheumatism pamoja na matatizo ya misuli.
“Baadhi ya watu wanaopata huduma hii huripoti kupungua kwa maumivu ya mwili, uchovu na msongo wa mawazo,” amesema Brenda.
Amesema pia sumu ya nyuki inaaminika kusaidia mzunguko wa damu pamoja na kuimarisha mfumo wa kinga ya mwili.
Mbali na tiba hiyo, banda la TFS pia limekuwa likitoa elimu kuhusu bidhaa mbalimbali zitokanazo na nyuki ikiwemo asali, nta pamoja na bidhaa za ngozi.
Baadhi ya wananchi waliotembelea maonesho hayo wamesema walikuwa hawajawahi kusikia kuhusu tiba ya udungwaji wa nyuki kabla ya kufika kwenye banda hilo.
“Nilikuwa najua nyuki ni kwa ajili ya asali tu, lakini leo nimeona hata tiba ipo,” amesema mmoja wa wageni waliotembelea maonesho hayo.
Hata hivyo, wataalamu wa afya wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa tiba za asili kufanyika chini ya usimamizi wa wataalamu kutokana na baadhi ya watu kuwa na mzio mkali wa sumu ya nyuki.
Maonesho ya Wizara ya Maliasili na Utalii yamezikutanisha taasisi mbalimbali kuonesha huduma, bidhaa na ubunifu unaohusiana na uhifadhi wa maliasili pamoja na utalii.
Soma