Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) limeendelea kushuhudia ongezeko la biashara huku mauzo yakifikia zaidi ya Tshs bilioni 9 katika biashara ya Mei 15, 2026.
Kwa mujibu wa ripoti ya soko hilo, jumla ya hisa milioni 1.28 ziliuzwa kupitia miamala zaidi ya 3,000.
Hisa za benki ziliongoza biashara hiyo, ambapo NMB na CRDB zilikuwa miongoni mwa kampuni zilizofanya vizuri zaidi siku hiyo.
NMB iliuza zaidi ya hisa 432,000 kupitia mfumo wa block trade, huku CRDB ikiongoza kwa shughuli nyingi kwenye soko la kawaida baada ya kuuza zaidi ya hisa 415,000 kwa wastani wa Tshs 2,720 kwa hisa.
Kampuni ya Tanzania Breweries Limited (TBL) nayo ilikuwa miongoni mwa kampuni zilizofanya biashara kubwa baada ya kuuza hisa 100,000 kupitia block trade.
Makampuni mengine yaliyofanya biashara ni pamoja na AFRIPRISE, Swissport Tanzania (SWIS), TOL Gases pamoja na Tanzania Portland Cement.
Ripoti hiyo pia imeonyesha kuwa biashara ya bondi za serikali iliendelea kukua, ambapo thamani ya miamala ilifikia zaidi ya Tshs bilioni 57.
Bondi hizo zilihusisha dhamana za miaka 5, 20 na 25, jambo linaloonyesha maendeleo kwa uwekezaji kwenye hati fungani za muda mrefu.
Kwa upande wa thamani ya soko, DSE imesema jumla ya thamani ya kampuni zote zilizoorodheshwa imefikia Tshs trilioni 33.26.
Wachambuzi wa masoko ya fedha wanasema kuongezeka kwa biashara ya hisa za benki kunaonyesha imani ya wawekezaji kwenye sekta ya fedha nchini.
Katika miaka ya karibuni, DSE imeendelea kuona ongezeko la ushiriki wa wawekezaji binafsi huku elimu kuhusu uwekezaji kwenye soko la hisa ikiongezeka nchini.