Serikali yatoa zaidi ya leseni 11,000 za madini ndani ya miezi tisa


Na Mwandishi wetu, Dodoma

Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini imetoa jumla ya leseni 11,674 za shughuli mbalimbali za madini katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026.

Idadi hiyo imevuka lengo lililokuwa limepangwa la kutoa leseni 11,463 katika kipindi hicho.

Taarifa hiyo imetolewa bungeni na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Kwa mujibu wa Waziri Mavunde, leseni nyingi zilizotolewa ni za uchimbaji mdogo wa madini, ambapo jumla ya leseni 8,878 zilitolewa kwa wachimbaji wadogo nchini.

Amesema leseni nyingine zilizotolewa ni pamoja na leseni 313 za utafutaji madini, leseni 21 za uchimbaji wa kati, leseni 41 za uchenjuaji madini, leseni 914 za biashara kubwa ya madini pamoja na leseni 1,507 za biashara ndogo ya madini.

Waziri Mavunde amesema serikali pia imeendelea kuchukua hatua dhidi ya leseni zilizokiuka masharti ya kisheria.

Leseni 111 za utafutaji madini pamoja na leseni 35 za uchimbaji wa kati zilipewa hati za makosa kutokana na kutolipa ada za mwaka na kushindwa kuendeleza maeneo yao ya uchimbaji.

Leseni 53 za utafutaji madini na leseni 29 za uchimbaji wa kati zilifutwa baada ya wamiliki wake kushindwa kurekebisha makosa yaliyobainika.

Serikali imeendelea kusimamia shughuli za uchenjuaji madini ambapo mitambo 52 ya kuchenjua dhahabu aina ya CIP/CIL, mitambo 509 ya Vat Leaching pamoja na mitambo 204 ya Elution ilikaguliwa katika mikoa 25 ya kimadini.

Serikali pia inaendelea kuimarisha usimamizi wa ufungaji wa migodi ili kuhakikisha maeneo ya migodi yanakuwa salama na yenye manufaa kwa jamii baada ya shughuli za uchimbaji kumalizika.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mipango minne ya ufungaji migodi ilijadiliwa lakini hakuna ulioidhinishwa kutokana na mapungufu mbalimbali ikiwemo kukosekana kwa taarifa za kitaalamu kuhusu uimara wa miamba pamoja na ukosefu wa maoni kutoka kwa wadau wa maeneo husika.