Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Serikali imesema itaendelea kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili wafanyabiashara nchini ili kuboresha mazingira ya biashara na kulinda usalama wa mitaji yao.
Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Aristides Mbwasi aliyemwakilisha Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga kwenye hafla ya utoaji wa tuzo za Kariakoo Business Awards.
Mbwasi amesema Serikali inatambua nafasi ya Kariakoo katika uchumi wa Tanzania kutokana na idadi kubwa ya wafanyabiashara na shughuli za biashara zinazofanyika kila siku.
Amesema Kariakoo imeendelea kuwa kitovu muhimu cha biashara kwa wafanyabiashara wa ndani na kutoka nchi jirani.
“Serikali itaendelea kusikiliza na kutatua changamoto za wafanyabiashara ili kuhakikisha wanapata mazingira salama, yenye utulivu na uwazi wa mitaji yao,” amesema Mbwasi.
Amesema wafanyabiashara wengi nchini wameanza na mitaji midogo lakini wameweza kukua kupitia biashara zinazofanyika Kariakoo.
Kwa mujibu wa Mbwasi, wafanyabiashara kutoka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki na Kati ikiwemo DRC, Rwanda, Burundi, Zambia, Malawi, Uganda na Comoro huingia Kariakoo kufanya biashara kila siku.
Akizungumzia ujenzi wa Soko Kuu la Kariakoo baada ya ajali ya moto iliyotokea miaka ya nyuma, amesema Serikali ilijenga upya soko hilo kwa gharama ya takribani Tshs bilioni 28.
Soko hilo sasa lina zaidi ya maduka 2,000 na limejengwa kwa kiwango kikubwa zaidi ili kuongeza usalama na mazingira bora ya biashara.
Mwenyekiti wa Kariakoo Business Awards, Zakayo Shushu amesema tuzo hizo zinalenga kutambua mchango wa wafanyabiashara pamoja na kuhamasisha ushindani wa kibiashara wenye weledi na ubunifu.
Wafanyabiashara wa Kariakoo wamekuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa biashara, ajira na uchumi wa Tanzania