Kigamboni Awards yaanza kuvuka mipaka ya Dar es Salaam

Tamasha la Kigamboni Awards linaendelea kukua kwa kasi huku waandaaji wake wakisema sasa wanalenga kulifanya kuwa moja ya matamasha makubwa ya filamu nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa Chama cha Waigizaji Wilaya ya Kigamboni na Mratibu Mkuu wa tamasha hilo, Mike Nondo, alipokuwa akizungumza kuhusu maandalizi ya msimu wa nne wa mashindano hayo ya mwaka 2026.

Amesema tofauti na misimu iliyopita, mwaka huu tamasha hilo limepanua ushiriki wake nje ya Wilaya ya Kigamboni na sasa linapokea washiriki kutoka mikoa mbalimbali nchini.

“Tunataka Kigamboni Awards iwe tamasha la kitaifa. Tunataka washiriki kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania waje kushindana hapa Kigamboni,” amesema Mike.

Kwa mujibu wa Mike, mikoa inayoshiriki mwaka huu ni pamoja na Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Tanga pamoja na Zanzibar.

Amesema hatua hiyo inaonyesha namna tamasha hilo linavyoendelea kukua na kupata imani kutoka kwa wadau wa filamu na sanaa nchini.

Mike amesema waandaaji wameendelea kufanya maboresho kila mwaka ili kuongeza ubora wa tamasha hilo na kuvutia washiriki wengi zaidi.

“Ukifanya kitu kilekile kila mwaka watu wanachoka. Ndiyo maana tumekuwa tukiboresha trophy, maandalizi ya event na hata sehemu ya kufanyia hafla,” amesema.

Amesema msimu wa tatu ulikuwa wa kihistoria baada ya washindi kuanza kupewa zawadi za fedha taslimu sambamba na trophy, jambo lililoongeza ushindani na hamasa kwa washiriki.

Kwa sasa, amesema tayari zaidi ya filamu 300 zimewasilishwa kupitia mfumo wa online huku zikiwa zimebaki siku chache kabla dirisha la usajili kufungwa.

“Hii inaonyesha watu wanaamini Kigamboni Awards na wanataka kuwa sehemu ya safari hii,” amesema.

Waandaaji pia wamesema wanaendelea kuboresha mifumo ya majaji na upigaji kura ili kuhakikisha haki na uwazi vinazingatiwa kwa washiriki wote.

Mbali na mafanikio hayo, Mike amesema changamoto ya upatikanaji wa wadhamini bado ipo, huku akieleza kuwa sekta ya sanaa bado inahitaji kupewa nafasi kubwa zaidi na wadau wa biashara pamoja na vyombo vya habari.

Hata hivyo, amesema matumaini yao ni kuona Kigamboni Awards inakuwa jukwaa kubwa la kukuza vipaji vya filamu nchini na kuifanya Kigamboni kuwa moja ya maeneo muhimu kwenye tasnia ya filamu Tanzania.

soma