Watanzania kuanza kuangalia uwekezaji nje ya nchi


Kwa miaka mingi, uwekezaji nje ya nchi lilikuwa jambo la matajiri wakubwa, wawekezaji wa kimataifa au Watanzania wanaoishi nje ya nchi (Diasporas).

Lakini sasa hali inaanza kubadilika.

Kupitia simu janja, internet na majukwaa ya kidijitali, baadhi ya vijana wa Tanzania wanaanza kufuatilia masoko ya hisa ya Marekani, biashara za mtandaoni, fedha za kidijitali pamoja na kampuni za kimataifa.

Majina ya kampuni kama Apple, Tesla na NVIDIA sasa yanaanza kujadiliwa hata kwenye makundi ya WhatsApp na Telegram ya vijana wa Tanzania wanaopenda uwekezaji na teknolojia.

Lakini pamoja na hamasa hiyo, swali kubwa linaendelea kubaki: Mtanzania anaweza kuwekeza nje ya nchi kihalali? Na sheria zinasemaje?

Kwa mujibu wa Benki kuu ya Tanzania, miamala yote ya fedha za kigeni nchini ipo chini ya usimamizi wa Benki Kuu kupitia sheria na kanuni za fedha za kigeni.

Kanuni hizo zinaruhusu Mtanzania kufanya uwekezaji nje ya nchi, lakini fedha lazima zipitie kwenye mfumo rasmi wa benki na taasisi zilizoidhinishwa.

Kwa vitendo, benki nyingi huomba maelezo ya chanzo cha fedha, sababu ya uwekezaji pamoja na nyaraka za biashara kabla ya fedha kuhamishwa nje ya Tanzania.

Hatua hizo zinaelezwa kuwa sehemu ya sheria za kuzuia utakatishaji fedha pamoja na kulinda akiba ya fedha za kigeni nchini.

Kwa sasa, ongezeko la vijana wanaofanya kazi mtandaoni limeanza kubadilisha mtazamo kuhusu uwekezaji wa kimataifa.

Baadhi yao hulipwa/hutarajia malipo kwa dola kupitia kazi za freelancing, programming, YouTube, forex pamoja na biashara za kidijitali.

Kadri teknolojia inavyorahisisha upatikanaji wa taarifa, Watanzania wengi zaidi wanaanza kufuatilia majukwaa ya uwekezaji ya kimataifa kama interactivebrokers.com.

Hata hivyo, wataalamu wa sheria na fedha wanaonya kuwa uwekezaji wa nje si rahisi kama unavyoonekana kwenye video za TikTok au Instagram.

Changamoto zinazotajwa ni pamoja na sheria za fedha za kigeni, kodi za kimataifa, usalama wa fedha, uthibitisho wa akaunti pamoja na hatari ya utapeli wa mtandaoni.

Majukwaa mengi ya kimataifa huhitaji nyaraka za makazi, akaunti za benki za kimataifa au mifumo mingine ambayo bado si rahisi kwa baadhi ya Watanzania.

Kadri biashara za kuvuka mipaka zinavyoongezeka Afrika Mashariki, kampuni za sheria za biashara nazo zinaanza kupata nafasi kubwa zaidi.

Miongoni mwa kampuni zinazotajwa kwenye masuala ya uwekezaji wa kimataifa ni bowmanslaw.com, ambayo imekuwa ikihusika kwenye ushauri wa uwekezaji, mikataba ya biashara, mergers pamoja na masoko ya mitaji ndani ya Afrika.

Kwa wawekezaji wakubwa, kampuni za sheria husaidia kuhakikisha sheria za Tanzania na nchi husika zinafuatwa pamoja na kusaidia masuala ya kodi na migogoro ya biashara.

Wachambuzi wa uchumi wanaamini Tanzania inaweza kushuhudia kizazi kipya cha wawekezaji wanaotazama zaidi ya mipaka ya nchi.

Lakini wataalamu wanasema uwekezaji wa nje unahitaji elimu ya fedha, uelewa wa sheria, uvumilivu pamoja na tahadhari kubwa dhidi ya hatari za kifedha.

Kwa sasa, fursa zinaongezeka. Lakini safari ya uwekezaji wa kimataifa bado ina sheria nyingi, ukaguzi mkubwa wa fedha na changamoto ambazo wengi hawazioni mwanzoni.