iTrust yazindua hatifungani ya Tshs bilioni 100


Na Mwandishi wetu

Kampuni ya iTrust Finance Limited imezindua rasmi programu ya hatifungani yenye thamani ya Tshs bilioni 100.

Hatua hiyo inaifanya iTrust kuwa kampuni ya kwanza ya udalali wa hisa na usimamizi wa mifuko ya uwekezaji nchini kutoa hatifungani ya kampuni.

Uzinduzi huo umefanyika Dar es Salaam kupitia awamu ya kwanza inayolenga kukusanya Tshs bilioni 15 pamoja na nafasi ya kuongeza Tshs bilioni 5 kulingana na mahitaji ya soko.

Kwa mujibu wa kampuni hiyo, hatifungani hiyo itakuwa ya miaka minne na italipa riba ya asilimia 13 kwa mwaka.

Malipo ya riba yatafanyika kila baada ya miezi mitatu bila makato ya kodi ya zuio.

Hatifungani hiyo inayojulikana kama “iTrust Bond” imeidhinishwa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) na ilifunguliwa rasmi Mei 18, 2026.

Inatarajiwa kufungwa Juni 12, 2026 kabla ya kuanza kuuzwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).

Kampuni hiyo imesema kiwango cha chini cha kuwekeza ni Tshs 500,000 ili kuwapa nafasi Watanzania wengi zaidi kushiriki kwenye uwekezaji huo.

iTrust imesema fedha zitakazopatikana zitatumika kuongeza uwezo wa utoaji wa mikopo, kuimarisha mifumo ya kidijitali pamoja na kuongeza mtaji wa kampuni.

Katika uzinduzi huo, Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Faiz Arab, pia alizindua programu ya simu ya “iTrust App”.

Programu hiyo itawawezesha wananchi kuwekeza kwenye hatifungani, hisa pamoja na mifuko ya uwekezaji kupitia simu.

iTrust Finance Limited ni taasisi ya huduma za kifedha inayosimamiwa na Benki kuu ya Tanzania pamoja na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA).

Mbali na udalali wa hisa, kampuni hiyo pia hutoa huduma za ushauri wa uwekezaji, usimamizi wa mifuko na huduma za kifedha zinazofuata misingi ya Sharia kupitia kitengo chake cha Imaan Finance.