Soko la Hisa la Dar es salaam (DSE) imesema soko la mitaji Tanzania linaendelea kukua huku teknolojia na ubunifu wa huduma za kifedha vikiongeza ushiriki wa wawekezaji wengi zaidi nchini.
Hayo yameelezwa katika hafla ya wadau wa sekta ya fedha na uwekezaji iliyowakutanisha viongozi wa soko la hisa, wasimamizi wa mifuko ya uwekezaji, mawakala wa hisa pamoja na taasisi mbalimbali za kifedha.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mtendaji Mkuu wa DSE, Peter Nalitolela, amesema Tanzania imeendelea kushuhudia hatua mpya katika maendeleo ya soko la mitaji na huduma za uwekezaji.
Amesema taasisi mbalimbali za kifedha zimeanza kupanua huduma zake kwa kuongeza usimamizi wa mifuko ya uwekezaji, ushauri wa kifedha pamoja na udalali wa hisa.
“Tumeona ukuaji mkubwa wa soko la mitaji kwa miaka ya hivi karibuni. Teknolojia imeongeza nafasi kwa wananchi wengi zaidi kushiriki kwenye uwekezaji,” amesema.
DSE ilieleza kuwa baadhi ya bidhaa mpya za uwekezaji zilizozinduliwa katika miaka ya karibuni zimeongeza fursa kwa wawekezaji wa ndani kupata huduma zinazofanana na masoko mengine ya kimataifa.
Soko hilo pia lilieleza mafanikio ya matumizi ya mifumo ya kidijitali inayowezesha wananchi kufuatilia na kufanya uwekezaji kupitia simu muda wowote.
Kwa mujibu wa viongozi hao, matumizi ya programu za kidijitali yamepunguza urasimu na kurahisisha wananchi kununua hisa, hatifungani pamoja na bidhaa nyingine za uwekezaji.
Wadau wa sekta hiyo walisisitiza umuhimu wa elimu ya fedha kwa wananchi ili kuongeza uelewa wa uwekezaji na ushiriki katika soko la mitaji.
Katika hafla hiyo pia ilielezwa kuwa thamani ya soko imeendelea kuongezeka ikilinganishwa na miaka ya nyuma, huku kampuni mbalimbali zikizidi kutumia soko la hisa kupata mitaji ya biashara na miradi ya maendeleo.